April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wawekezaji Norway, Uingereza
waitwa sekta ya miundombinu

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa amewaalika wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchi za Norway na Uingereza kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali za uchumi na huduma hapa Tanzania hususani kwenye sekta ya ujenzi wa miundombinu.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano uliowaleta pamoja watendaji wa taasisi za Serikali na Ujumbe wa Wawekezaji na wafanyabiashara 37 kutoka nchini za Norway na Uingereza ulioratibiwa na Norwegian-African Business Association na Kampuni ya Invest Africa kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Prof Mbarawa aliwahakishiwa wawekezaji hao kuwepo kwa mazingira mazuri ya uwekezaji na kufanya biashara.

Amesema uwekezaji katika sekta ya miundombinu hususani ujenzi wa barabara na reli itasaidi kufungua fursa lukuki za kibiashara na uwekezaji kwenye nyanja zingine za ki uchumi na kijamii zilizopo hapa nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt Maduhu Kazi (kulia) akijadiliana jambo na viongozi na wawakilishi wa wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Norway na Uingereza muda mfupi baadaya ya mkutano uliowaleta pamoja Watendaji wa taasisi za Serikali na Ujumbe wa Wawekezaji na wafanyabiashara 37 kutoka nchini za Norway na Uingereza ulioratibiwa na Norwegian-African Business Association na Kampuni ya Invest Africa kwa kushirikiana na TIC).

“Mpaka hivi sasa kwa upande wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa wa SGR umefikia asilimia 97 lakini hii inatoa haitoshi kwa kuwa kuna baadhi ya maeneo nchini bado yanahitaji huduma ya reli kwa kuwa ni maeneo yenye shughuli kubwa za uzalishaji”, amesema Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa ameongeza kuwa uboreshaji wa miundombinu haiitaji nguvu ya serikali pekee kwa kuwa serikali inatoa fursa kwa wadau na wawekezaji kuwekeza nchini jambo ambalo limekuwa likifanywa hata na mataifa yaliyoendelea.

“Ninachukua nafasi hii kuwahamasisha muje kwa wingi na serikali yetu sikivu iliyo chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inawathamini wawekezaji hasa kwenye kuwashirikisha kwenye miradi mikubwa ya miundombinu ambayo itakwenda kuifungua nchi kimaendeleo na kutoa fursa kubwa ya ajira nchini”, amesema Prof. Mbarawa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji TIC, Dkt. Maduhu Kazi mbali ya kuwahakikishia ushirikiano mkubwa wafanyabiashara na wawekezaji hao, alibainisha kuwa kituo hicho kitaendelea kutengeneza mazingira mazuri ili kuvutia zaidi na kurahisisha shughuli za uwekezaji nchini.

“Ninapenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha sana kuwekeza nchini hasa kwenye maeneo ya fedha, uvuvi, usafirishaji, kilimo na uchukuzi, na niwatoe wasiwasi kwa kuwa serikali imeweka mazingira mazuri zaidi ya uwekezaji”, Amesema Dkt. Maduhu.

Dkt. Maduhu ameongeza kuwa, “Serikali inamatarajio makubwa na nyinyi kuja kuwekeza nchini na hii inadhihirisha kwa kuwa Rais wetu amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha uwekezaji na kuitangaza nchini jambo ambalo limepokelewa vizuri na wawekezaji”.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ,Prof Makame Mbarawa akijadiliana jambo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Norwegian –African Business Association (NABA), Bw Eivind Fjeldstad (katikati) na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt Maduhu Kazi mara baada ya Waziri Mbarawa kufungua mkutano uliowaleta pamoja Watendaji wa taasisi za Serikali na Ujumbe wa Wawekezaji na wafanyabiashara 37 kutoka nchini za Norway na Uingereza ulioratibiwa na Norwegian-African Business Association na Kampuni ya Invest Africa kwa kushirikiana na TIC).

Aidha akizungumza kwa niaba ya Wafanyabiasha na wawekezaji hao, Afisa Mtendaji Mkuu wa Norwegian-African Business Association (NABA) Bw. Eivind Fjeldstad amesema lengo la ujio wao ni kujionea fursa zilizopo nchini na huku akibainisha nia yao ya kuja kuwekekeza kwenye sekta za kilimo, uvuvi, usafirishaji na uchukuzi.

“Hii ni nafasi nzuri kwetu kuwepo hapa, na ni faraja kwetu kuwepo kwenye nchi yenye fursa nyingi ambazo zikitumiwa ipasavyo zitakwenda kuleta tija kwa taifa hili”, amesema, Fjelstad.

Matunda ya ujio ya wawekezaji haya pia yanachangiwa na juhudi kubwa inayofanywa na serikali hasa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye kuitangaza nchi na kuvutia wawekezaji mbalimbali kuja kuwekeza jamba ambalo linaangaziwa kuwa lenye kuleta matokeo chanya kwa taifa kwa siku za usoni.