-Amuweka kikaangoni Mkuu wa Takukuru, ataka RPC kushughulika.
Na Moses Ng’wat, TimesMajira Online, TUNDUMA
HALMASHAURI ya Mji wa Tunduma imewasimamisha kazi Afisa Manunuzi wa Halmashauri hiyo, Ibrahim Lulimo na Mhandisi wa Ujenzi Japheti Chota wakituhumiwa katika ubadhilifu wa mamilioni ya fedha kwenye ujenzi wa soko la wafanyabiashara wadogo maarufu wamachinga ambalo serikali ilishatoa kiasi cha Sh.Milioni 383.
Ujenzi wa soko hilo ambalo linajengwa katika kata ya Majengo mjini Tunduma umesimama kwa muda mrefu sasa kwasababu hakuna fedha kwenye akaunti.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Philemon Magesa, alimweleza Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk. Francis Michael kuwa alichukua hatua ya kuwasimamisha kazi maofisa hao baada ya ripoti ya Mkaguzi wa Ndani kubaini kuna vifaa vilinunuliwa lakini havikupelekwa eneo la mradi.
“Mkaguzi wa ndani alishafanya ukaguzi mradi huu baadhi ya mapungufu yaliyoonekana kwenye mradi huu ni baadhi ya vifaa kununuliwa lakini havikuoneka ‘saiti’ ambavyo ni nondo,saruji, mchanga ,kokoto na mawe na hatua nilizochukua ni kuwasimamisha baadhi ya watumishi ambao ni Ofisa Manunuzi na Mhandisi aliyekuwa akisimamia,”alisema Magesa.
Magesa alisema baada ya kuwasimamisha kazi maofisa hao alikabidhiwa suala hilo kwa Mkuu wa Wilaya Momba, Fakh Lulandala, ili aweze kuchukua hatua zaidi kwa kuwa yeye ana vyombo vya dola.
Baada ya majibu hayo ya Mkurugenzi, Mkuu wa Mkoa alimtaka Mkuu wa wilaya atoe majibu je baada ya kukabidhiwa majina ya maofisa hao waliosimamishwa alichukua hatua gani.
Mkuu wa Wilaya Momba, Lulandala alisema baada ya kukabidhiwa majina hayo aliwakamata wahusika na Kisha kuwakabidhi kwa Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kituo maalum Tunsuma ili achunguze zaidi suala hilo.
Naye Afisa wa TAKUKURU kituo maalum Tunduma Benedict Kaombwe aliyeitwa na Mkuu wa Mkoa ili kujibu swali juu ya hatua zilizochukuliwa na taasisi hiyo alijibu kwa kifupi kuwa uchunguzi bado unaendelea wa suala hilo.
Hata hivyo, majibu hayo ya Afisa wa TAKUKURU hayakumfurahisha Mkuu wa Mkoa ambaye alihoji inakuweje suala hilo ambalo tayari ripoti ya Mkaguzi imeeleza bayana uchunguzi wake uchukue zaidi ya miezi miwili.
“TAKUKURU uchunguzi zaidi ya miezi miwili ujue hizi ni hela za umma, mnachunguza nini halafu mbaya zaidi hadi Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya inachukua hatua…hapana hapa lazima kuna vitu haviko sawa,” alihoji Mkuu wa Mkoa na kuongeza .
“Nakuelekeza vinginevyo nitaongea na wakubwa zao huko, umepewa kazi ya kuwachunguza watu kwa tuhuma za ubadhirifu nataka haraka tupate majibu kwani hizi ni fedha zilizotolewa na rais kwa ajili ya wamachinga, sasa nyie hapa Tunduma mnaona mmeletewa hela za kula, haiwezekani uchunguze zaidi ya miezi miwili wakati mkaguzi ameshatoa ripoti yake,” alifoka Dk. Michael.
Kufuatia hali hiyo,Mkuu wa Mkoa Dk.Michael, aliagiza TAKUKURU kupeleka haraka ripoti yao ya uchunguzi ofisini kwake pamoja na ripoti ya Mkaguzi wa Ndani.
Aidha, Dk.Michael alimwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Theopista Mallya kuwatafuta watuhumiwa wa ubadhirifu huo na kuwahoji ili hatua za kisheria zianze kuchukuliwa dhidi yao.
Pia aliwataka Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha watu wote wanaofanya ubadhirifu katika wilaya hiyo wasifumbiwe macho na badala yake washughulikiwe kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.
“Hii haikubaliki na kwa watumishi wauma hatua zichukuliwe kwa mujibu wa taratibu za utumishi na wale wasio watumishi nao pia hatua zichukuliwe kwani hatuko tayari kuona Sh.Milioni 400 zinaishia hapa kwa majengo haya, yaaani watu hata hatuogopi,” alisema.
Mradi wa soko la wamachinga katika Halmasjhauri ya Mji wa Tunduma unajengwa katika kata ya Majengo mjini Tunduma ambapo utagharimu zaidi ya Sh.Bilioni 6 hadi kukamilika kwake.
Katika utekelezaji wa mradi huo tayari serikali imetoa Sh. milioni 383 za awali na halmashauri kupitia mapato ya ndani imeongeza Sh. Milioni 28 kwa ajili ya uchimbaji wa kisima na mfumo wa umeme lakini hadi sasa ujenzi umesimama na benki hakuna salio lolote.
More Stories
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti