January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtumishi wa Mungu, Mchamungu Mwasakikoba akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) jana jijini Dar es Salam.

Watumishi wa dini wadanganyifu watakiwa kutubu.

Na. Bakari Lulela
,TimesMajira,Online

MITUME, Manabii na Watumishi wa dini wanaotumia udanganyifu ama nguvu za kiza kuendesha ibada zao katika makanisa mbalimbali hapa nchini, wametakiwa kutubu na kurudi kwenye njia sahihi ya kumuabudu mungu.

Akitoa tamko hilo jijini Dar es Salaam jana Mtumishi wa Mungu, Mchamungu Mwasakikoba amesema wasipotubu ifikapo agosti 31 mwaka huu wanaweza kupata matatizo ya kiakili.

“Watu hawa ni hatari sana kwenye jamii wameonekana kuwaathiri watu kwa kiwango kikubwa kiroho na kimaisha ambapo wanapaswa kutubu waziwazi mbele ya waliowaathiri kwa maana washirika wao kwa kukiri kuwa walikuwa wakiwadanganya,” amesema Mwasakikoba

Amesema kuwa kwa kipindi kirefu watumishi hao wamekuwa wakitoa huduma alizoziita za kishetani kwa lengo la kujipatia vipato visivyo halali.

“Hizi ni huduma za kilaghai zinazofanywa kwa kumshirikisha shetani kwa kuchukua sadaka na matoleo mbalimbali ambapo imekuwa ni utamaduni kwa watumishi kuweza kujinufaisha.
,”amesema

Katika hatua nyingine Mtumishi huyo amempongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa jitihada mbalimbali za kuliletea Taifa la watanzania maendeleo na nchi kufikia katika uchumi wa kati kwa kutambua kuwa kazi ndio msingi mkubwa wa kukuza na kuboresha maisha kwa watu wote.

“Kipindi kifupi cha miaka mitano ameweza kuleta mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali kupelekea kuwa miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kwa kasi katika maendeleo na kumtanguliza mungu katika majukumu ya kazi zake,” amesema