May 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu mkuu Ofisi ya Waziri mkuu Kazi,Vijana,Ajira na wenye Ulemavu Andrew Masawe (kulia) akiongea wakati wa kufunga kikao kazi kati ya maofisa wa OSHA na CMA mkoani Morogoro (kushoto) ni Kaimu mtendaji Mkuu OSHA,Khadija Mwenda .

OSHA na CMA zatakiwa kudumisha ushirikiano

Na Bakari Lulela,TimesMajira,Online

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Vijana,Ajira na Wenye ulemavu,Andrew Masawe amezitaka Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa kazi (OSHA) pamoja na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kuendelea kushirikiana katika kuhakikisha kunakuwepo na Usalama na Afya katika maeneo ya kazi.

Akizungumza wakati wa kufunga kikao kazi kati ya Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa kazi (OSHA) pamoja na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) mkoani Morogoro, Masawe amesema OSHA na CMA zina mahusiano yanayotegemeana na ili eneo la kazi liweze kuwa na usalama na afya nzuri kwa wafanyakazi na kusiwe na shida sehemu za kazi .

Amesema taasisi hizo zinatakiwa kuhakikisha haki inatendeke, sheria, kanuni na miongozo iweze kufanyiwa kazi vizuri.

Masawe ameongeza kuwa sehemu za kazi zinapaswa kutokuwa na migogoro na wafanyakazi wanatakiwa kufanya kazi kwa amani.

Aidha Masawe amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2019/2020 CMA imeweza kusuluhisha jumla ya zaidi ya migogoro elfu 10 ambayo ni sawa na asilimia 81 huku migogoro zaidi ya elfu 6 sawa na asilimia 77 ikitolewa uamuzi.

Kaimu mtendaji mkuu wa OSHA Bi Khadija Mwenda amesema lengo la kikao kazi hicho ni kujadiliana namna gani ya kutatua migogoro sehemu za kazi ili kupunguza migogoro isiyo ya lazima sehemu za kazi.