Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online Tunduma
WATU saba wamepoteza maisha na wengine 13 kujeruhiwa katika ajali iliyotokea eneo la mpakani, mjini Tunduma, wilayani Momba baada ya Lori linalodaiwa kufeli breki kugonga kundi la watu walikuwa kwenye harakati za kumnasua dereva wa bodaboda aliyenasa chini ya gari aina ya Fuso (IT) baada ya bodaboda huyo kugongana na fuso hilo.
Lori hilo baada ya kugonga kundi hilo la watu pia liliendelea kugonga magari mengine likiwemo gari dogo la abiria (Hiace) lililokuwa na abiria ndani pamoja na bajaji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Theopister Mallya, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kwamba ilitokea majira ya saa 12:45 katika eneo hilo la mpakani Mjini Tunduma.
Amsema katika ajali hiyo, watu watano wote wanaume walifariki papo hapo, huku watu wengine wawili walifariki wakiwa wanapatiwa matibabu baada ya kukimbizwa katika kituo cha Afya Tunduma.
Pia amesema majeruhi wote 13 walikimbizwa katika kituo cha Afya Tunduma ambapo 10 walitibiwa na kuruhusiwa huku watatu wakiendelea na matibabu kutokana na majeraha mbalimbali waliyoyapata.
Kamanda Mallya amesema kati ya watu hao saba (wote wanaume) waliofariki, sita wameweza kutambuliwa na ndugu zao na miili yao imehifadhiwa katika kituo cha Afya Tunduma.
Amewataja marehemu waliotambuliwa kuwa ni Baraka Mwankenja (25) maarufu kama Fally Ipupa ambaye ni dereva wa bodaboda aliyefariki akitibiwa kituo cha afya, Aizack Kasebele (28), Baraka Lutufyo (23), Fred Karagwe(28), Emmanuel Mlay (24) na John Kapizo (25) wote wakazi wa Tunduma.
Amewataja majeruhi wanaoendelea na matibabu katika kituo hicho cha afya Tunduma kuwa ni Zainab Hassan (43), Oliva Ngusa (38), Hassan Kwambaza (45) dereva wa Lori.
More Stories
Bodaboda wamchangia Rais Samia Mil 1 ya fomu ya Urais
HAYA HAPA MATOKEO YOTE FORM II NA DARASA LA IV
Ufaulu waongezeka matokeo ya Darasa la Nne na Kidato cha Pili