May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watoto watano wafariki dunia kwa kuzama kwenye dimbwi la maji

Na Esther Macha, TimesmajiraOnline, Mbeya

WATOTO watano wamefariki dunia mkoani Mbeya baada ya kuzama ndani ya dimbwi la maji wakati wakiogolea katika shamba la Kakao lenye ukubwa wa ekari nne katika Kijiji cha Ngeleka kata ya Makwale Wilaya ya Kyela mkoani hapa.

Akizungumzia tukio hilo Kaimu Kamanda wa polisi Mkoani Mbeya, Abdi Issango amesema tukio hilo limetokea April 7 ,mwaka huu katika Kitongoji cha Katagho Kijiji cha Ngeleka kata ya Makwale tarafa ya Ntebela.

Aidha Kaimu Kamanda Issango amesema kuwa watoto hao walifariki dunia wakati wakipatiwa matibabu katika zahanati ya uhai Baptist iliyopo wilayani Kyela.

“Watoto hawa walizama ndani ya dimbwi la maji lililopo kwenye shamba la kakao lenye ukubwa wa ekari nne”amesema Kamanda Issango.

Hata hivyo Issango amewataja Watoto walifariki kuwa ni Raphael Mwaikale (05) mwanafunzi wa darasa la kwanza shule ya msingi Ngeleka,Carolina Mwamkamba (ambaye ni pacha (06) mwanafunzi wa darasa la kwanza shule ya msingi Makwale,Lightness Kakenda (05) mwanafunzi wa chekechea shule ya msingi Ngeleka na kalebu Mwaikombe (05) Mwanafunzi wa chekechea shule ya msingi. Ngeleka.

Akielezea zaidi Kaimu Kamanda huyo amesema Uchunguzi wa awali umebaini kuwa watoto hao walienda kuogelea kwenye dimbwi lililojaa maji kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha ndipo walizidiwa na maji na kuzama.

Amesema kuwa watoto walipozidiwa maji walipiga kelele kuomba msaada wa kuokolewa na wananchi lakini tayari walikuwa katika hali mbaya na kukimbizwa katika Zahanati ya Uhai Baptist hata hivyo walifariki dunia wakiwa wanaendelea kupatiwa matibabu.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kutoa wito kwa wazazi na walezi kuchukua tahadhari kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwa kuhakikisha wanaweka uangalizi mzuri kwa watoto wao ili kuwalinda dhidi ya maafa yatokanayo na mvua.