November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watoto wasiokuwa na haja kubwa wafanyiwa upasuaji

Na Esther Macha,Timesmajira,Oline,Mbeya

HOSPITALI ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili imewafanyia upasuaji watoto 15 ambao walikuwa na changamoto ya kutokuwa na sehemu ya haja kubwa.

Wakizungumza na gazeti hili mara baada ya kumalizika kwa upasuaji wa watoto hao, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Dino Mwaja amesema wamepata mafanikio makubwa, ikiwemo kuhudumia zaidi ya wagonjwa 25 katika kliniki yao, ambapo watoto zaidi wamefanyiwa upasuaji wa sehemu ya haja kubwa.

Aidha Dkt.Mwaja amesema mafanikio hayo siyo ya kubeza na wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Serikali ya awamu ya sita ,Wizara ya afya ,Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya pamoja na timu nzima iliyoshiriki upasuaji huo.

Daktari Bingwa wa Watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili,
Victor Ngota, amesema kwa ushirikiano na Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya wamewezesha kufika na kutoa huduma za kibingwa kwa watoto ambao walikuwa wanahitaji  huduma za upasuaji wa sehemu ya haja kubwa ambayo hawakuwa nayo.

Akifafanua zaidi Dkt.Ngota amesema wagonjwa ambao wameonwa ni zaidi ya 25 na wamefanyiwa upasuaji watoto 15.

Madaktari wakifanyia upasuaji watoto hao

Amesema watoto hao walitakiwa kupelekwa Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu, lakini wamefanyiwa upasuaji jijini Mbeya na hivyo kupunguza gharama kubwa ya kusafiri pamoja na malazi.

“Asilimia kubwa ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji ni wale ambao walizaliwa na changamoto ya kutokuwa na sehemu ya haja kubwa tumeweza kuwasaidia watoto hao na wanaendelea vizuri,”amesema Dkt .Ngota.

Daktari Bingwa wa Usingizi na Ganzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Lukansola Mabusi, amesema waliweza kutoa dawa hiyo kwa usalama kwa watoto pamoja na kuwajengea uwezo watoa huduma katika hospitali hiyo ya Kanda Mbeya.