May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watendaji NIDA watakiwa kurahisisha utaratibu wananchi kujiandikisha

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Watendaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA),wametakiwo kuweka utaratibu utakao wezasha wananchi na wageni wanaostahili kujiandisha kuhakikisha wanaandikishwa bila usumbufu.

Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Elikana Balandya wakati uzinduzi wa zoezi la ugawaji wa vitanbulisho hivyo uliofanyika Februari 19, mwaka huu ambapo ameeleza kuwa wakumbuke kuwa watakutana na watu tofauti tofauti ikiwemo wenye mahitaji maalumu,wazee, walemavu na wajawazito hivyo wanatakiwa kuweka utaratibu mzuri ili kuwaondolea usumbufu.

“Ni jukumu letu sisi watendaji ambao tumepewa dhamana na kuhakikisha kwamba tunawaandikisha wananchi kujipanga namna ya kurahisisha uandikishaji pamoja na utoaji wa huduma hii,kwa wale wenye mahitaji ya msingi na maalumu ili kuhakikisha wanapata huduma hiyo bila usumbufu wowote,”ameeleza Balandya.

Balandya ameeleza kuwa ni ukweli usiopingika wananchi wengi waliandikishwa na kukaa muda mrefu bila kupata vitambulisho vyao hivyo kulikuwa na malalamiko ya kuchelewa kupatikana kwa vitambulisho hivyo.

Ambapo malalamiko hayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa na jambo hilo lilikuwa kero kwa wananchi wengi wa Mkoa wa Mwanza wameandikishwa lakini vitambulisho havikuweza kupatikana kwa muda.

Hivyo ameeleza kuwa Mkoa wa Mwanza unavitambulisho vilivyotengenezwa zaidi ya laki 7,idadi hii ni kubwa anaamini kwamba inaenda kumaliza kero ambayo wananchi wengi wanakumbana nayo ya kutokupata vitambulisho vya NIDA.

“Tunaamini kwamba taasisi yetu hii ya NIDA inaendelea kutengeneza vitambulisho kwa ajili ya kutoa kwa wananchi kwa wakati,hivyo waendelee kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha wananchi wote wanahitaji kuandikishwa wanaandikishwa na wanapata vitambulisho vyao kwa wakati,”.

Pia ameeleza kuwa suala la vitambulisho vya taifa lipo kisheria,sheria ya uandikishwaji ya utambuzi wa raia inapatikana katika sura namba 36, iliofanyiwa maboresho mwaka 2012 kifungu namba 7 inayoeleza kila raia mwenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea anayeishi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamtaka aombe kuandikishwa kwenye daftari la mamlaka ya vitambulisho vya taifa ili kwanza apatiwe namba ya utambulisho na baadae kupatiwa kitambulisho cha taifa.

Hivyo ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza kujitokeza kwa wingi katika zoezi la kujiandikisha kwanza na katika zoezi la uchukuaji vitambulisho ambavyo vimetolewa zaidi ya laki saba ili visiendelee kukaa ofisini kwa watendaji wa NIDA au wa serikali za mitaa.

“Vitambulisho hivi vitapelekwa kwenye maeneo yetu katika ofisi za serikali za mitaa na orodha itakuwa imebandikwa pale,kwaio mwende mkachukue hivyo vitambulisho orodha itakuwa imebandikwa kwenye ofisi za vijiji,mitaa ili Kila mwananchi ambaye amejiandikisha asome jina lake na akikiona achukue kitambulisho chake kwa wakati visiendelee kubaki katika ofisi zetu,”ameeleza Balandya na kuongeza kuwa

“Na kwa wale ambao hawajiandikisha ila wanasifa wajitokeze kwa wingi ili waweze kupata haki yao kusajili na kutambuliwa katika zoezi hili na watoe ushirikiano pia ni jukumu la kila mmoja atakaye pewa kitambulisho kuhakikisha tunavitunza ili vitumike kwa mahitaji mbalimbali pale vitakapo hitajika,”.

Kwa upande wake Ofisa Msajili wa NIDA Daudi Abdallah ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwa ofisi za usajili na utambuzi za Wilaya kwa Mkoa wa Mwanza mamlaka ili kuwa na lengo la kusajili wananchi zaidi ya milioni 1.7,mpaka sasa umefanikiwa kusajili na kutambua wananchi,wageni wakazi kwa pamoja idadi yao imefikia zaidi ya milioni 1.5 ambayo ni sawa na asilimia 84.3 ya malengo.

Kati ya hao walio sajiliwa zimezalishwa namba za utambulisho zaidi ya milioni 1.3 na kuzalisha vitambulisho hapo awali zaidi ya laki 7, ambavyo vimeisha sambazwa katika ofisi za serikali za mitaa katika Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Mwanza.Daud ameeleza kuwa changamoto iliopo ni muitikio mdogo wa wananchi kuchukua vitambulisho vyao ambavyo tayari vimeisha zalishwa na kusambazwa kwa muda mrefu katika ofisi za watendaji wa mitaa.

Hali ambayo imechangia mrundikano wa vitambulisho hivyo kutishia lengo la serikali kutofikiwa la kila mwananchi,mgeni makazi na mkimbizi anasajiliwa na kupata namba ya utambulisho ya taifa hatimaye kupata kitambulisho cha taifa kama zao la mwisho.

Sanjari na hayo ameeleza changamoto nyingine ni wananchi kujitokeza kusajiliwa pale anapokumbana na hitaji linalomlazimu kuwa na namba ya utambulisho au kitambulisho cha taifa.

“Hali hii imekuwa ikizua malalamiko kwani muombaji hatambui kuwa baada ya kusajiliwa zipo hatua mbalimbali muhimu ambazo lazima zipitiwe kabla ya kuzalishiwa namba ya kitambulisho hatimaye kitambulisho cha taifa,”ameeleza Daud.