September 18, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watatu wafariki,44 wajeruhiwa katika ajali wakitoka kuzika

Na Moses Ng’wat, Mbozi

WATU watatu wamefariki na wengine 44 kujeruhiwa baada ya gari lililokuwa limebeba watu 54 waliokuwa wakirejea kutoka kwenye mazishi kupinduka katika eneo la Kona ya Veta, Kijiji cha Nsenya, Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe.

Ajali hiyo imetokea jioni ya Septemba 17, 2026, baada ya gari aina ya Mitsubishi Fuso, lenye namba za usajili T 177 DJY, kupata hitilafu likiwa njiani, kuyumba na hatimaye kupinduka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga, akizungumza kwa njia ya simu usiku huu, amesema kuwa gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Gervas Msongole, mkazi wa Mlowo, ambaye alikimbia baada ya ajali na anaendelea kutafutwa na polisi.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa ajali hiyo ilisababishwa na kukatika kwa ‘centre bolt’, hali iliyofanya gari kuyumba na kupinduka.

Kamanda Senga amesema majeruhi hao 44 walipelekwa katika Hospitali za Rufaa ya Mkoa, Wilaya ya Mbozi na Hospitali binafsi ya Ilasi kwa ajili ya matibabu, ambapo watatu walifariki dunia wakati wakipatiwa huduma.

Amesema kati ya majeruhi hao 44, majeruhi 22 walipatiwa matibabu na kuruhusiwa.

Amesema waliopoteza maisha ni wanaume wawili na mwanamke mmoja, huku majina yao yakiwa bado hayajafahamika.

Mmoja wa majeruhi, Baraka Simchimba, Mkazi wa Hasanga, amesema akiwa sehemu ya watu waliokuwa kwenye Fuso amesema anejeruhiwa kichwani na kuvunjika kidole cha mwisho cha mkono wa kushoto amesema alishtuka na kukuta gari imeanguka chini na baada ya hapo alijikuta Hospitali.

Aidha, Senga ametoa tahadhari kwa wamiliki na madereva wa magari ya mizigo kuacha kubeba abiria, akisisitiza kuwa magari hayo hayapaswi kutumika kusafirisha abiria.