April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watanzania waunga Mkono Mikakati ya Kupunguza Uzalishaji wa Methane

Na Penina Malundo, timesmajira

WATANZANIA wameonekana kuunga mkono kwa kiasi kikubwa mipango inayolenga kupunguza uzalishaji wa gesi ya methane na kushughulikia mabadiliko ya hali ya hewa.

Taarifa iliyotolewa jana kwa waandishi wa habari na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Global Methane Hub, Marcelo Mena amesema shirika lao limefanya tafiti juu ya hali ya uzalishaji wa methane duniani na kujumuisha nchi 17 katika mabara sita, umetoa ufahamu wa jinsi jamii inavyoiona hali ya mazingira na njia za kisheria za kurekebisha hali hiyo.

Amesema matokeo ya utafiti huo yanaonesha kwamba asilimia 83 ya washiriki kutoka Tanzania wanapendelea sera zinazolenga kupunguza uzalishaji hatari wa methane ambapo kati yao, asilimia 49 wanaunga mkono mkubwa, kiwango ambacho ni cha juu zaidi kuliko nchi nyingine zilizofanyiwa utafiti.

Amesema asilimia 87 ya watanzania wanaamini kwamba shughuli za binadamu ndio sababu kuu ya mabadiliko ya hali ya hewa, ikionesha ufahamu mkubwa wa umuhimu wa kuchukua hatua za kupunguza athari hizo.

Mena amesema utafiti huo pia unaonesha asilimia 88 ya washiriki kutoka Tanzania wanapendelea sheria zinazolenga kupunguza upotevu wa chakula na utupaji sahihi wa taka za kikaboni kwani
taka hizo ni moja ya vyanzo vikuu vya uzalishaji wa methane.

“Kupunguza uzalishaji wa methane ni njia ya haraka zaidi ya kupunguza ongezeko la joto duniani na kudhibiti athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwani utafiti huu tulioufanya unaonesha kwamba wale wanaoathiriwa zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa ndio wanaotoa uungaji mkono mkubwa kwa jitihada za kupunguza methane,”amesema.

”Utafiti huo pia unathibitisha, uungaji mkono wa mikakati ya kupunguza gesi ya methane ambayo umebaki imara licha ya tofauti katika ufahamu wa awali wa gesi hiyo katika nchi zilizofanyiwa utafiti,”amesema Mena.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa kampuni ya BSG,
Natalie Lupiani, amesisitiza kwamba takwimu hizo zilizotolewa na Shirika la Global Methane Hub ni ishara nzuri kwamba watu wanaunga mkono serikali zao katika kuchukua hatua za kuwalinda dhidi ya ongezeko la joto duniani.

Alisema Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi tatu zilizoathiriwa zaidi, pamoja na Brazil na Kenya, huku karibu nusu ya washiriki wakiripoti athari kali katika maisha yao ya kila siku.

Naye Mwenyekiti wa Jopo la Kitaalam la Sayansi la Hali ya Hewa na Hewa Safi (The Climate and Clean Air Coalition Scientific Advisory Panel), Drew Shindell, amesisitiza umuhimu wa kupunguza uzalishaji wa methane mara moja ili kuzuia jamii dhidi ya athari mbaya za uchafuzi wa hewa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Ripoti inaonesha kuwa kupungua kwa kiasi kikubwa katika ongezeko la joto kunaweza kutokea kupitia juhudi za kupunguza methane kwa asilimia 45, ambayo itasaidia kuleta mustakabali bora na kufikia malengo ya kimataifa ya hali ya hewa.