Na Mwandishi Wetu, TimesMajira, Online Mbeya
BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Nchini(TADB) imeadhimisha wiki ya wateja kwa kuhimiza ushirikiano endelevu wa wateja wake pamoja na wadau mbalimbali katika sekta za kilimo,mifugo na uvuvi kama njia ya kuhamasisha uwekezaji zaidi katika sekta hizo muhimu kwa uchumi wa Taifa.
Akizungumza na wateja pamoja na wadau wengine wa benki hiyo Mkoani Mbeya, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege amesema benki yake imetumia wiki ya wateja kuhamasisha watanzania hususani vijana kuchangamkia fursa lukuki zilizopo kwenye sekta za kilimo,mifugo na uvuvi.
“Sisi kama TADB tunayo dhamana kubwa ya kuchagiza maendeleo na ukuaji wa sekta hizo ili ziweze kutoa mchango stahiki katika ukuaji wa uchumi wa Taifa sambamba na kumwezesha mkulima,mfugaji na mvuvi kuongeza uzalishaji na kukuza kipato chake,” amesema Nyabundege.
Nyabundege ambaye yupo katika mikoa ya Nyanda za juu kusini mwa Tanzania hakusita kueleza kuwa mikoa ya Iringa,Mbeya, Njombe, Songea,Songwe na Rukwa ipo katika nafasi nzuri ya kuzalisha zaidi mazao ya chakula na biashara na hivyo kuimarisha mnyororo wa thamani ya mazao hapa nchini.
“Nimefurahi kuonana na kuwasikiliza wadau mbalimbali wa benki ambao wameweza kutoa ushuhuda wao namna benki ilivyoweza kuwasaidia kuongeza uzalishaji na thamani ya bidhaa zao,” ameeleza Nyabundege.
Nyabundege akiwa nyanda za juu kusini alifanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Serikali za mikoa hiyo, wakulima na wafugaji ambao walionyesha imani kubwa kwake na kumuomba kuwaunga mkono sambamba na kutembelea miradi iliyodhaminiwa na benki hiyo.
“Nimefarijika kujionea mwenyewe nini kinachofanyika na kuwasikiliza wakulima wenyewe changamoto wanazokabiliana nazo na kuweza kuwa na picha nzuri ya namna benki itakavyoweza kutatua changamoto hizo,” amesema Nyabundege nakuongeza kuwa benki itaendelea kuwa karibu nao na kutoa ushirikiano ili kufanikisha miradi yao.
Amesema TADB kama benki ya Serikali inajukumu la kutekeleza malengo ya Serikali yaliyosababisha kuanzishwa kwa benki hiyo na kuwahakikishia kuwa benki yake imejipanga kuwafikia wakulima , wafugaji na wavuvi kwa wakati na ufanisi kubwa ili wapate mitaji na kutekeleza miradi yao.
Amesema wiki ya wateja imesaidia kumpa nafasi ya kuwasikiliza wadau na pia kubadilishana uzoefu ili kuboresha huduma za benki na kuwafanya wadau waweze kunufaika kwa uwepo wa benki hiyo hapa nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Kampuni ya Forever Investment inayojihusisha na kilimo cha Kahawa Mkoani Songwe, Jane Daima ameshukuru benki kwa kumwalika kwenye maadhimisho ya wiki ya wateja amesema imekuwa ni faraja kwake kuonana na kujadiliana mambo mbalimbali na uongozi wa juu wa benki ya TADB.
“Hii ni nafasi pekee kwake na wadau wengine wakilimo kuweza kukutana na viongozi wa ngazi za juu za benki na kufanya mazungumzo yenye tija katika kuboresha huduma hususani upatikanaji wa mikopo itayaosaidia kuboresha shughuli zetu za kilimo,” amesema Daima
Akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano mwezi Aprili mwaka huu Jijini Dodoma mara baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan alieleza umuhimu kuiongeza fedha zaidi benki ya TADB ili iweze kutoa mikopo mingi yenye riba nafuu kwa wakulima, wavuvi na wafugaji hali itakayosaidia kuongeza uzalishaji wa mazao ambayo yatakwenda kuwa malighafi katika viwanda vilivyopo nchini.
Alisema Serikali yake imedhamiria kuifanya Tanzania nchini ya viwanda ifikapo mwaka 2025 na sekta za kilimo,mifugo na uvuvi zina nafasi kubwa katika kufanikisha azma hiyo ya ujenzi wa viwanda.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi