December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watanzania waaswa kuunge mkono dhamira ya Rais Samia

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

DHAMIRA njema ni maono mema kwa ajili ya kesho njema yenye ustawi. Kuwa na dhamira njema ni jambo moja na kuitimiza dhamira hiyo njema ni jambo jingine.Ni vigumu kuitimiza dhamira njema peke yako pasipo kuungwa mkono na wadau wengine.

Kuna msemo wa Kiswahili usemao kuwa kila mmoja ni kiungo kwa mwenzake. Ndiyo! huwezi kufanya jambo peke yako na kufanikisha pasipo kupata ushirikiano thabiti kutoka wengine ikiwa jambo hilo linahusu maslahi ya wengi.

Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan,akiwa ni kiongozi mkuu wa nchi,ameonesha dhamira njema katika kuifanya Tanzania kupiga hatua kubwa kwenye nyanja za demokrasia,maendeleo na usawa wa kijinsia.

Mwandishi wa makala hii amezungumza na Mkurugenzi wa Asasi ya Kiraia ya Wezesha Mabadiliko ya mjini Mororogo,Lusako Mwakiluma kwa lengo la kupata maoni juu mwenendo wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, na nini kifanyike kwa lengo la kuunga mkono dhamira yake njema ya kuipeleka Tanzania kwenye uchumi mzuri, kuimarisha demokrasia, uhuru wa vyombo vya habari na kuifanya kuwa nchi yenye kujali misingi ya uongozi wenye kutoa uwiano wa uwakilishi wa 50 kwa 50 kati ya wanawake na wanaume kwenye vyombo vya maamuzi.

Lusako anaanza kueleza kuwa taasisi yake ya Wezesha Mabadiliko, ina dhima kubwa ya kuchochea mabadiliko chanya katika jamii na kwa ajili hiyo hufurahia mabadiliko yoyote yanayotokea kwenye jamii hiyo katika nyanja za uongozi, uchumi, elimu, demokrasia na uhuru wa kiraia wenye lengo la kuimarisha ustawi wa jamii.

Anasema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ameanza vizuri kuiongoza nchi na kwa muda wa miezi miwili akiwa madarakani ametoa mwelekeo chanya wa mustakabari wa Taifa.

Mwakiluma anaitaja hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan, wakati alipohutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania kwa ujumla kwa lengo la kutanabaisha vipaumbele vya Serikali yake ya awamu ya sita kuwa ilionesha mweleko chanya juu ya ustawi wa Taifa.

Anasema kuwa Watanzania waliipokea kwa furaha hotuba hiyo na imewafariji mno kwa kuwa wameona Tanzania inakwenda kung’ara kisiasa na kiuchumi huku kukiwa na dalili njema za kuulinda Muungano wetu.

Anasema kuwa hata salamu mpya ambayo rais ameitambulisha inaonesha dhamira njema juu ya Muungano wetu.

“Salamu inayotamkwa ‘Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku ikijibiwa, Kazi iendelee’ ni dalili tosha kuwa ipo dhamira ya dhati inayoendeleza dhamira za viongozi wa awamu zilizopita ya kudumisha Muungano wetu ambao ni tunu yetu na inasisitiza kufanya kazi kwa mwendelezo usiokoma kwa lengo la kujiletea maendeleo na kuondokana na utegemezi, “ anasema Mwakiluma.

Mwakiluma anasema kuwa uadilifu wa Rais Samia,sio wa kutilia shaka kwani kabla ya kuwa Rais, amewahi kuaminiwa na viongozi wakuu wa nchi yetu katika nafasi mbali mbali za uongozi serikalini na kwenye chama CCM.

“Rais Samia aliwahi kunukuliwa akisema kuwa aliyemuibua kwenye uongozi ni Rais mstaafu wa Zanzibar, Aman Abeid Karume, ambaye alimteua kuwa Waziri katika serikali ya Mapinduzi. Rais Mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, naye pia alimwona anafaa na kumteua kuwa Waziri katika serikali ya Muungano na baadae, hayati Rais wa awamu ya tano Dkt. John Pombe Magufuli, akamchagua kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi a mwaka 2015 na hatimae kuwa makamu wa Rais kwa kipindi cha miaka zaidi ya mitano..” anasema Mwakiluma.

Mwakiluma anoangeza kusema kuwa sasa Samia Suluhu Hassani ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,ni wazi kuwa historia hiyo ya Mama Samia Suluhu Hassan, inatutafakarisha na kutupa somo na funzo kubwa watanzania hususani wanawake.

“Somo kubwa ambalo Watanzania hususani wanawake tunapaswa kulitambua na kuliishi ni somo linahusu umuhimu wa uadilifu katika uwajibikaji. Mama Samia Suhusu Hassan anabebwa na kiwango chake cha juu cha uadilifu na uwajibikaji bila kuchoka wala kukata tamaa.” anaeleza Mwakiluma.

Mwakiluma anasema kuwa uwezo wa Rais Samia wa kusimamia kwa weledi majukumu anayopewa, uzalendo na kushirikiana na wengine katika usimamizi bora wa rasilimali ni sifa zilizombeba na kumfikisha hapo alipo.

“Dhamira ya Rais Samia inabaki kuwa ile ile ya kuwajibika kwa nguvu na maarifa,kusimamia rasimali za nchi, nidhamu na kiu ya maendeleo isiyokwisha,hivyo tunachotakiwa kukifanya sisi Watanzania ni kumuunga mkono kwa nguvu zote ili kutimiza dhamira hiyo njema ambayo itatuvusha na kutuletea ustawi mkubwa” anasema Mwakiluma.

Mwakiluma anazitaja sifa nyingine za Rais Samia ambazo zinaonesha wazi dhamira yake njema juu ya Taifa Tanzania kuwa ni pamoja na kukubali kukosolewa na uwezo wa kutambua michango ya wengine na kutaka kuwajumuisha watu wenye uwezo wa kiutendaji bila kujali itikadi zao za vyama katika kulijenga Taifa.

“Kukubali kushauriwa sambamba na majadiliano kwenye masuala yenye tija kwa Taifa ni sifa za ziada za Rais wetu. Stara,kujiheshimu, kuheshimu wengine na kutia nia na lengo la wapi anataka Taifa lifike ni miongoni mwa sifa zitakazoliinua Taifa Tanzania endapo watanzania tutaamua kwa dhati kumuunga mkono rais wetu,” anaeleza Mwakiluma.

Mwakiluma anaikumbuka kauli ya Rais Samia aliyoitoa wakati anahutubia bunge kwa mara ya kwanza kuwa ‘Ukinizingua nami nitakuzingua”! kuwa ni kauli ambayo inaonesha kwamba pamoja kwamba ni mwanamke hataki ifike hatua ya watu wakachukulia udhaifu wa wanawake kupitia kukariri mfumo dume kutenda vitendo viovu vitakavyofifisha dhamira yake njema ya kuijenga Tanzania.

Anasema kuwa Rais Samia kwa kauli hiyo ameonesha jinsi ambavyo hayupo tayari kukumbatia watendaji magoi goi, wala rushwa na wazembe kazini.
“Rais Samia amenonesha ni kwa kiwango gani amedhamiria kupambana na wahujumu uchumi, wezi, wabadhirifu, magogoi na wanaokumbatia urasimu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku, tunapaswa kumuunga mkono.” Anasema Mwakiluma.

UTEUZI WA WANAWAKE KATIKA NAFASI ZA UONGOZI

Mwakiluma anasema kwa muda mrefu taasisi ya Wezesha Mbadiliko, imekuwa ikitilia mkazo na kuhamasiha wanawake kujitokeza katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi. Amekuwa akifanya hivyo kwa kuzingatia kuwa sera ya uwiano wa asilimila 50 kwa 50 kati ya wanawake na wanaume kwenye vyombo vya uwakilishi na vyombo vya maamuzi inatekelezwa kikamilifu.

“Rais,Samia Suluhu Hassan, katika hotuba yake ya kwanza bungeni na pia amenukuliwa mara nyingi akisema kuwa katika utawala wake atahakikisha wanawake wenye sifa na vigezo anawapa nafasi katika uongozi kwa kuwateua katika nafasi mbali mbali,” anaeleza Mwakiluma.

ANGALIZO KWA WANAWAKE WATAKAO TEULIWA

Mwakiluma anasema kuwa hapa nchini kwetu wapo wanawake wengi wenye sifa na vigezo vya kuwa viongozi. Anasema Rais ameliona hilo hivyo anawaasa wanawake walioteuliwa na watakaoteuliwa katika nafasi mbali mbali za uongozi kuwajibika kwa kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa yenye ubunifu kwa lengo la kuchochea kasi ya ukuaji wa maendeleo.

“Wanawake watakao teuliwa wasibweteke kwa kuwa wamepata nafasi za uongozi wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii ili aliyewateua asijutie kuwateua katika nafasi hizo.”

Mwakiluma anasema kuwa huu ni wakati wa wanawake kutimiza kilio chao cha miaka mingi hivyo kwa wale watakaopata nafasi za uongozi wanapaswa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kuidhihirishi jamii kuwa wanawake wanaweza kufanya kile ambacho pia wanaume wanaweza.

“Kauli ya Rais Samia kuwa wanawake wameumbwa na ubongo unaoweza kufanya kazi sawa sawa na wanaume ituamshe wanawake na kututia ari, shime, na iwe kichocheo cha kufanya mabadiliko chanya kwa kuongeza nguvu katika uwajibikaji kwenye shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi ili tuweze kushiriki sawasawa katika kusukumu gurudumu la maendeleo ya nchi yetu,” anaeleza.

MWENENDO WA WABUNGE

Mwakiluma anaunga mkono kauli ya Rais Samia aliyotoa bungeni iliyowata wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujikita katika hoja za msingi na zenye tija kwa mustakabari wa Taifa kwa kuwa wananchi wa Tanzania wanakabiliwa na vikwazo vingi vya maendeleo.

“Ukweli ni kwamba wabunge ndio sauti ya Wananchi, ndio wawakilishi wetu. Wana dhima kubwa ya kuisimamia serikali na kutoa uwakilishi wa changamoto za wananchi bungeni ili zitatuliwe na serikali. Kundi hili la wawakilishi ni kundi muhimu kwa ajili ya kuisukuma agenda yenye dhamira njema ya Rais Samia ya kuifanya Tanzania kuwa yenye ustawi katika nyanja za uchumi, elimu, afya, miundombinu na mazingira,” anasema Mwakiluma.