December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Watanzania tujivunie rekodi ya utendaji wa Rais Samia

MAONI YA MHARIRI, TimesMajira Online

MACHI 19, mwaka huu aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akichukua nafasi hiyo kufuatia kifo cha Rais John Magufuli.

Mara baada ya kuapishwa alitoa hotuba fupi iliyobeba ujumbe mzito akisema;

“Huu siyo wakati wa kutazama mbele kwa mashaka, bali ni wakati wa kutazama mbele kwa matumaini na kujiamini. Si wakati wa kutazama yaliyopita bali ni wakati wa kutazama yajayo. Si wakati wa kunyoosheana vidole bali ni wakati wa kushikana mikono na kusonga mbele.

Tofauti na viapo vya awali ambavyo nilivila kwa faraja, nderemo, vifijo na bashasha tele, leo nimekula kiapo cha juu kabisa katika nchi yetu adhimu Tanzania nikiwa na majonzi tele na nchi ikiwa imetandwa na wingu jeusi la simanzi kubwa. Nimekula kiapo katika siku ya maombolezo,”

Amesema; “huu ni wakati wa kufutana machozi na kufarijiana ili tuweke nguvu zetu za pamoja kujenga Tanzania mpya ambayo mpendwa wetu Rais Magufuli aliitamani.”

Hotuba hiyo ya Rais Samia inaonesha wazi kwamba dhamira yake kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake ni kujenga Tanzania mpya. Sisi kama chombo cha habari hatuna mashaka na uwezo wa Rais Samia kutokana na rekodi yake ya uongozi.

Kutokana na rekodi yake ya uongozi iliyotukuka kila sehemu alipoongoza ni wazi kila jambo ambalo lipo mbele yake atalitekeleza kwa ufanisi wa hali ya juu.

Japo chini ya uongozi wake atakabiliwa na mambo mbalimbali mbele yake ikiwa ni pamoja na kupanga safu ya viongozi watakaomsaidia kutimiza ndoto na maono yake, kutokana na uwezo wake tunaamini kazi hiyo ataifanya kwa ufanisi wa hali ya juu.

Aidha, kwa uwezo wake tunaamini atahakikisha miradi ya mikakati iliyoanzishwa na msaidizi wake inatekelezwa kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kudumisha nidhamu kwa watumishi wa umma.

Miradi hiyo ya kimkakati ni pamoja na ujenzi wa bwawa kubwa la kufua umeme la Nyerere, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ujenzi wa miundombinu ya barabara.

Jambo jingine ni kujenga umoja wa kitaifa na mshikamano

Maeneo mengine ni ni kuimarisha misingi ya demokrasia, kuimarisha misingi ya utawala bora na kuhakikisha vitendo vya ufisadi vilivyokuwa vimekithiri miaka ya nyuma.

Eneo lingine ambalo tunaamini atalifanyia kazi ni kilio cha wafanyabiashara kutozwa kodi kubwa kinyume na biashara zao.

Pamoja na changamoto zilizopo tuna imani kwamba kazi hiyo itakuwa nyepesi kwake kutokana na uwezo wake.

Pia kazi hiyo itakuwa nyepesi zaidi iwapo atatengeneza safu ya viongozi wazuri watakaomsaidia katika majukumu yake. Mwelekeo wake utategemea viongozi atakaowateua kwa ajili ya kumsaidia katika majukumu yake mbalimbali.

Hiyo inawezekana kwa sababu amekuwa mwanafunzi mzuri chini ya mtangulizi wake ambaye ameweza kufanya mambo makubwa ikiwemo kutekeleza miradi ya kimkakati.