May 12, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watandaza nyaya za umeme chini ya maji Ziwa Tanganyika

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online. Rukwa

WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) kupitia Nakuroi Investment Co. Ltd, inayotekeleza mradi wa awamu ya tatu mzunguko wa kwanza unaendelea na kazi ya kulaza nyaya chini ya maji katika Ziwa Tanganyika, ili kufikisha umeme Kisiwa cha Mandakerenge kilichopo Kata ya Kipili wilayani Nkasi Mkoa wa Rukwa.

Kazi hiyo itakayogharimu zaidi ya sh. bilioni saba ni la kipekee kufanyika katika Ziwa Tanganyika na Mikoa ya Kanda ya Ziwa, hali iliyofanya Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Mwanza na timu kutoka makao makuu ya shirika hilo, kufika katika eneo hilo na kujifunza utandazaji wa nyaya hizo ili kuja kuutumia ujuzi huo kufikisha umeme Kisiwani Ukerewe Mkoa wa Mwanza.

Akizungumza wakati wa kushiriki kulaza nyaya hizo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo amesema tukio hilo linaonesha ni kwa namna gani serikali inavyowathamini wananchi wake na kuzingatia haki zao za kupata huduma za kijamii sawa na watu wanaoishi katika maeneo mengine ya nchi.

Amewapongeza wazamiaji wazawa wanaofanya kazi hiyo, TANESCO Mkoa Rukwa na Mkandarasi wa Mradi ambapo aliwaomba wananchi wa Kisiwa na Kijiji cha Mandakerenge, kuutumia umeme huo vizuri ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda vya kuchakata samaki na mashine za kusaga na kukoboa.

“Serikali ya Tanzania inathamini wananchi popote pale walipo na umeme huu, utakwenda kila mahali ndani ya vijiji vyetu vya Mkoa wa Rukwa, baada ya kufikisha umeme katika Kisiwa cha Mandakerenge itakuwa ni takriban vijiji 181, vitakuwa vimefikiwa na umeme.

“Nimeambiwa huyu Mkandarasi Nakuroi, amebakiza kama vijiji viwili, vitatu ili vitimie vijiji 184 ambavyo vitakuwa vinapata umeme na vijiji vinavyobaki kama 155, hivi vijiji vitapata umeme ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na nusu,” amesema.

Amesema katika ya vijiji hivyo 155 vilivyobaki, 125 vimeingizwa katika mradi wa awamu ya tatu mzunguko wa pili na vijiji 30, vimeingia kwa maombi maalumu na hivyo kufanya jumla ya vijiji vya mzunguko wa kwanza na wa pili kuwa 339, ambavyo ni idadi ya vijiji vilivyopo mkoani Rukwa.

Kwa upande wake Meneja wa TANESCO Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Yusuf Ismail amesema kazi hiyo ilitakiwa kukamilika ndani ya wiki nne, lakini kutokana na ushiriki mzuri wa wanakijiji katika mradi, hali nzuri ya hewa ziwani pamoja na kasi ya kazi hiyo huenda kazi hiyo itamalizika chini ya muda uliopangwa.

Naye mwakilishi wa mkandarasi wa mradi huo wa REA mkoani Rukwa, Mhandisi Pascal Ndunguli amesema kwa upande wao wamekabidhiwa kukamilisha mradi huo katika vijiji 137 na kati ya hivyo, 135 tayari vimewashwa umeme na hivyo kubakiwa na vijiji viwili kimojawapo kikiwa ni hicho cha Kisiwa cha Mandakerenge, ambacho wanatazamia kukimaliza kabla ya mwezi wa sita mwaka huu.

Katika ziara hiyo alikuwepo mwakilishi wa wavuvi na wanakijiji wa Kijiji cha Mandakerenge, Seif Seba ambaye ameishukuru serikali kwa kufikisha umeme katika kijiji hicho.

“Tunatoa shukurani za dhati kwa serikali yetu kwa kutujali kwa suala la kutuletea umeme hapo kisiwani na tunaiahidi serikali, kuwa tutaulinda huu waya na hakutatokea athari ya namna yoyote,” amesema.

Kisiwa cha Mandakerenge kipo umbali wa kilomita 1.2 kutoka nchi kavu, ambapo shughuli kubwa za wanakijiji wa kisiwa hicho ni uvuvi na TANESCO, wametandaza waya wenye urefu wa kilomita 1.7 kutoka nchi kavu kwenda kisiwani, ili wanakijiji hao nao wafaidike na mradi huo.