April 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof. Mganilwa ataka mfumo rasmi kuwatambua wabunifu

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online, Dodoma

MKUU wa Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Mhandisi Profesa Zacharia Mganilwa ameitaka Serikali kuweka mfumo wa kuzitambua bunifu za wazawa na kuziendeleza.

Aidha, Profesa Mganilwa alisema kuwa kwa hatua walipofikia wabunifu wazawa wanatakiwa kuungwa mkono na Serikali na kuwandeleza ili bunifu zao ziwe na tija.

Prof. Mganilwa aliyasema hayo jijini hapa mwishoni mwa wiki katika kilelele cha mashindano ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) yaliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

” Ni kweli vijana wetu wameonesha uwezo mkubwa katika kubuni vitu vya Kisayansi, Serikali inatakiwa iweke mfumo mzuri wakuwaendeleza ili wabunifu hao waweze kuchangia Uchumi wa nchi,” amesema Mkuu huyo wa Chuo.

Mkuu wa Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Mhandisi Profesa Zacharia Mganilwa akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya MAKISATU yaliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma mwishoni mwa wiki.

Aidha kwa upande wa NIT, Mkuu huyo wa Chuo alisema wanafunzi wa Chuo hicho walikwenda katika maonesho hayo na ubunifu wa sensor ambayo inafungwa kwenye mabasi ilikuweza kumuelekeza abiria wapi anakwenda.

“Hii sensor inafungwa katika mabasi kama ya mwendokasi ambayo kazi yake nikuonesha basi linaenda wapi pindi basi hilo linapoingia kituoni, ” amesema Prof. Mganilwa.

Aidha Mkuu huyo wa Chuo alisema teknolojia nyingine waliyokwenda nayo katika mashindano hayo ni maski ambayo hutumika kuvuta hewa ya oxygen (Oxjeni) kwenye ndege wakati inapokuwa angani kuanzia futi 20.

“Unajua Ndege ikipaa juu kama futi 20,hewa yao oxjeni huwa inapungua hivyo maski hiyo husaidia kuvuta hewa ya oxjen,” alisema Mkuu huyo.

Mashindano hayo ya MAKISATU yaliyoenda sambamba na maonesho ya wabunifu yalianza Mei 6 nakumalizika jana.

Akiongea wa kati anafunga maonesho hayo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameziagiza taasisi na mamlaka ambazo zinashiriki kuendeleza wabunifu wachanga zihakikishe zinawawezesha kubiasharisha ubunifu na uvumbuzi wao.

Mkuu wa Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Mhandisi Profesa Zacharia Mganilwa akisisitiza jambo katika maonyesho ya MAKISATU yaliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma mwishoni mwa wiki. Katikati ni Afisa Uhusiano wa Chuo hicho Ngusekela David.

“Taasisi za sayansi na teknolojia; vyuovikuu; taasisi za utafiti na maendeleo; na mamlaka mbalimbali kama SIDO, VETA na DON BOSCO ambazo kwa na mna moja ama nyingine zinashiriki kuendeleza wabunifu wachanga ziwasaidie kubiasharisha ubunifu na uvumbuzi wao,” amesema.

Amesema kuwa uendelezwaji wa wa bunifu na wavumbuzi ufanyike kwa kasi na ufanisi mkubwa ilikuhakikisha matunda ya jitihada zinazofanywa na Wizara ya Elimu, Sayansi naTeknolojia za kuwaibua nakuwatambua wabunifu wachanga zinazaa matunda.

“Nitoe wito kwa taasisi zote kutumia ubunifu na uvumbuzi unaozalishwa nchini kama nyenzo muhimu wakati wakuandaa nakutekeleza mipango mbalimbali inayoandaliwa katika sekta zote, iwe za huduma au uzalishaji, ilikuongeza tija na kasi ya maendeleo ya Taifa letu,” amesema.

Pia amezitaka taasisi za elimu ya juu na zile za utafiti na maendeleo zishirikiane kwa karibu na sekta binafsi, hasa ya viwanda, naziweke utaratibu wa kuendeleza teknolojia zinazozalishwa nchini na kuhamasisha matumizi yake ili kuongeza kasi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Mkuu wa Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Mhandisi Profesa Zacharia Mganilwa

“Nia ya Serikali ni kuona ubunifu na uvumbuzi wa teknolojia zinazozalishwa na wabunifu wachanga unatoa mchango mkubwa katika kuzalisha ajira mpya, kuongeza kipato kwa wabunifu na kuchangia katika pato la Taifa.” amesisitiza.

Waziri Mkuu alisema ni vema iandaliwe kwa namna ambayo itawawezesha wahitimu kuwa wabunifu na mwisho wa siku waweze kutumia ubunifu huo kujitengenezea ajira zao wenyewe na ikiwezekana, wawaajiri wengine.

Ameeleza kuwa kuhusu suala la hatimiliki za wabunifu, Waziri Mkuu amesema anatarajia kuona mabadiliko ya haraka kwenye eneo hilo kwani hadi sasa idadi ya maombi yaliyowasilishwa kutoka Tanzania ni ndogo sana ikilinganishwa na maombi kutoka nchi jirani.

Awali Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe.Omar Kipanga amesema kuwa maonesho hayo ni moja ya mkakati wa wizara hiyo wa kuibua wabunifu na kukuza teknolojia miongoni mwa vijana. “Hii tunaamini itasaidia ukuaji wa uchumi wa nchi na kuongeza fursa kwa wabunifu kujipatia kipato,” amesema.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Godfrey Mulisa amesema kuwa Shirika hilo kwa kushirikiana na COSTECH wameandaa mradi mwingine ujulikanao kama UFUNGUO ambao utazinduliwa Jumatatu ijayo ukiwa na lengo la kuendeleza ubunifu miongoni mwa vijana.

Hata hivyo amewapongeza washiriki wa mashindano hayo kwa kupeleka kazi zao za ubunifu na kuamua kuzishindanisha.