May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watalii kutoka Morogoro,Dodoma watembelea Hifadhi ya Tarangire

Doreen Aloyce,TimesMajira Online,Manyara

Watalii wa ndani nchini wapatao 70 kutoka mikoa ya Morogoro na Dodoma wametembelea hifadhi ya Taifa ya Tarangire kujionea vivutio vilivyopo.

Ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kupitia sekta ya utalii na kuhamasisha utalii wa ndani na kimataifa kupitia filamu ya The Royol Tour aliyoizindua hivi karibuni nchini Marekani,

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mwishoni mwa wiki hii ,mara baada ya kufika katika hifadhi ya Tarangire,ziara hiyo ambayo imeandaluwa na Ofsi ya Tanapa Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na wadau wa utalii,wamesema utalii ni sehemu ya kuondoa msongo wa mawazo unachochewa na afya ya akili kutokana na changamoto wanazokumbana nazo.

Dinna Mola(70) kutoka Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma na Matrida Mande kutoka Morogoro wamesema wamejifunza mambo mengi kupitia Hifadhi ya Tarangire ikiwemo tabia za wanyama,kwani tangu kuzaliwa kwao hawajawahi kuona kwa macho simba,twiga na wanyama wengine zaidi ya kuwaona kwenye runinga.

“Kutembea kwenye mbunga za wanyama ni kuondoa msongo wa mawazo nimepata ya kuwahadithia wajukuu zangu niwasihi watanzania na wazee wenzangu watembelee mbuga za wanyama waondokane na mawazo ya kwamba wazungu ndiyo wanapaswa kutembelea,”amesema Dinna.

Kwa upande wa vijana waliopata fursa ya kutembelea hifadhi hiyo akiwemo Munna Amidu na Gidion Mbata,wamesema kuwa utalii ni njia ya kujifunza tamaduni mbalimbali na kuwasihi vijana watumie muda wao kutembelea hifadhi badala ya kutumia pesa zao kwenye sehemu za starehe ambazo zinawaingiza kwenye maisha hatarishi na mashindano.

Nae Ofisa Uhifadhi Daraja la Kwanza wa Hifadhi ya Tarangire Godfrey Mwakapeje, amesema kuwa hifadhi hiyo ni ya kipekee ambayo inaongoza kuwa na idadi kubwa ya wanyama hasa tembo ambao uvutia watalii ukilinganisha na maeneo mengine.

Amesema kuwa kupitia filamu ya The Royal Tour imeleta tija ambayo imesaidia wageni kutoka ndani na nje ya nchi kuwa na muamko wa kutembelea hifadhi na kwa mwaka 2022/2023 zaidi ya watalii milioni moja wamepatikana tofauti na hapo nyuma.

“Kati ya hao Watanzania ni laki nne na arobaini(440,000) japo idadi bado iko chini ila kutokana na uhamasishaji huu tutafanikiwa hasa katika utoaji elimu wa viingilio kwani watanzania wengi wamekuwa wakihofia,”amesema Mwakapeje.

Akizungumza juu ya ziara hiyo Ofisa Mhifadhi Mkuu Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (Tanapa) ofisi ya Dodoma Fredrick Malisa,amesema utalii huo ni muendelezo wa kampeni ya kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ya kutangaza utalii wa ndani kwa watoto kwa wakubwa ambao umeleta muamko mkubwa.

Amesema kuwa juhudi za Rais Samia Suluhu Hassani zimepelekea ofisi za Tanapa Dodoma kupitia Kamishna Saimon Mwakilema ameendelea kuiongezea nguvu ofisi hiyo ili iweze kutangaza utalii kuanzia Makao Makuu ya nchi na kuelekea kwenye hifadhi na imeleta matokeo makubwa.

“Nitoe wito kwa Watanzania waendelee kutembelea hifadhi mbalimbali na kufanya utalii ambao utawasaidia kujenga mahusiano na watu, kuburudika na kuelimika,”.

Hata hivyo zoezi hilo la kuhamasisha watanzania kutembelea hifadhi za wanyama na vivutio vyake linaendelea chini ya uratibu wa ofisi ya Tanapa Dodoma.