May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watakiwa kutoa elimu usafi wa mazingira kuwakinga na magonjwa ya kuhara

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Dkt.Samson Marwa ametoa wito kwa wahudumu wa afya katika vituo vyote vya kutolea huduma ndani ya Halmashauri hiyo kuweka utaratibu wa kutoa elimu ya usafi wa mazingira ili kuepuka magonjwa ya kuhara na kipindupindu ambayo yameanza kutokea kwa mikoa jirani.

Dkt.Marwa ametoa wito huo katika kikao kazi cha idara hiyo kilichofanyika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kilichohokuwa na malengo ya kufanya tathimini ya utekelezaji wa huduma za afya zilizotolewa kuanzia Januari hadi Septemba 2023 sambamba na kujadili changamoto na kuzipatia ufumbuzi na kuboresha huduma hizo.

“Kuchukua tahadhari ya kipindupindu ni muhimu na sisi kama wataalam wa afya tunawajibika kuelimisha jamii juu ya majanga hayo hasa nyakati hizi za mvua ili wazingatie Usafi wa mazingira,”amesema Dkt. Marwa.

Dkt.Marwa amesisitiza suala la wahudumu wa afya kutoa elimu za masuala ya kiafya kwa jamii hasa lishe bora ambayo ndio inamjenga mtu kuwa imara kiakili .

“Jamii inapaswa kufahamu mchanganyo wa makundi matano ya vyakula, wanga, protini, mbogamboga,matunda, sukari na mafuta bila kusahau maji kwa kuzingatia vipimo sahihi vyenye tija sio kula tu ilimradi kushiba,” amesema Dkt.Marwa

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa mkoa Ester Maliki ambaye ni Katibu wa Afya Mkoa wa Mwanza wakati alipohudhuria kikao hicho amewaasa Watumishi wa Idara ya Afya Halmashauri hiyo kuwajibika ipasavyo kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi kila mmoja kwa nafasi yake ili kuleta matokeo chanya katika huduma za afya.

“Kila mtu awajibike kwa nafasi yake,mvae umiliki wa kila kinachofanyika kwenye maeneo yenu,usimamizi wa miradi mbalimbali ,ukusanyaji na usimamizi wa mapato kwenye vituo vyetu ni jukumu la wote kikubwa ni kugawana majukumu ili mambo yaende kwa mpangilio mzuri,” amesema Ester.

Ester ametoa pongezi kwa kazi nzuri inayoendelea katika idara ya afya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ambapo amesema kuwa kazi hiyo ya huduma za afya ni wito hivyo wazidi kuipenda na kuifanya kwa bidii zaidi ili huduma ziwe bora zaidi.

Naye Katibu wa Afya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Emila Msangi,amesisitiza suala la ukusanyaji wa mapato kwa watumishi vituoni na kufanya kazi kwa umoja kwa manufaa ya wote.

“Kadri mnavyokusanya ndivyo mtakavyokuwa huru kutumia kwa matumizi yenu yenye tija katika maboresho ya utoaji huduma vituoni,ipo haja ya kubuni mbinu zaidi za kuwavutia wateja wetu,” amesema Emila

Taarifa mbalimbali za kiafya kama vile hali ya lishe,malaria,kifua kikuu,huduma za ustawi wa jamii zimewasilishwa na kujadiliwa lengo ikiwa ni kuboresha utoaji wa huduma.