April 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Mkoa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti akihutubia Baraza la Madiwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo kwenye kikao cha kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zilizoibuliwa katika halmashauri hiyo. (Picha na Allawi Kaboyo).

Watakiwa kusalimisha mamilioni ya fedha za umma ndani ya siku saba

Na Na Allawi Kaboyo, Biharamulo

MKUU wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti ametoa siku saba kwa watumishi wa Halmashauri ya wilaya Biharamulo waliokusanya fedha na kushindwa kuzipeleka benki wawe wamezipeleka kabla ya hatua kali za kinidhamu hazijachukuliwa dhidi yao.

Gaguti ametoa agizo hilo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo lililolenga kujibu hoja za Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambazo miongoni mwazo ni makusanyo ya fedha zaidi ya shilingi milioni 224 ambazo hazikupelekwa benki.

Amesema kuwa, licha ya halmashauri hiyo kufanya vizuri na kupata hati safi bado suala la ukusanyaji wa mapato ni changamoto ambapo aliongeza kuwa, wapo watendaji ambao wanakusanya fedha, lakini hawazipeleki benki na kupelekea halmashauri kuendelea kuandamwa na mzimu wa kutofikia malengo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani.

“CAG ametoa hoja mbalimbali kuhusu halmashauri hii na nyingi zinalalia masuala ya fedha, natoa siku saba kwa watendaji ambao wamehusika na kutopelekwa fedha hizi wawe wamezirejesha mara moja na kwenye hili sitanii kabisa tutakuja kuonana wabaya kwenye fedha za umma,”amesema Gaguti.

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Biaharamulo wakimsikiliza mkuu wa mkoa wa Kagera wakati wa Baraza la madiwani la halmashauri hiyo lililofanyika leo likiwa na lengo la kujadili hoja zilizoibuliwa na CAG juu ya halmashauri yao. (Picha na Allawi Kaboyo).

Aidha, alimemuomba mwenyekiti wa halmashauri hiyo kuitisha kikao kingine maalumu ambacho kitakuwa na agenda za kuangalia mwenendo mzima wa watumishi ndani ya halmashauri hiyo ili hatua husika ziweze kuchukuliwa pale itakapostahili.

“Mwenyekiti nataka kabla ya baraza hili kumaliza muda wake niitiwe kikao kingine mahususi kwa ajili ya madiwani pamoja na watumishi wote ili kuweza kuchukua hatua nyingine za kinidhamu kwa watumishi ambao wameonyesha vitendo vya ubadhirifu wa fedha za umma, lakini na mienendo mibaya,”alisisitiza Mkuu wa mkoa.

Kwa upande wao madiwani wakichangia kwa nyakati tofauti kwenye hoja za hizo za CAG wameitaka halmashauri kumalizia miradi mbalimbali ambayo wananchi tayari wameshaweka nguvu zao hasa vyumba vya madarasa ili kusaidia watoto kusomea katika mazingira ambayo ni mazuri na salama kwa ajili ya maisha yao ya baadae.