May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watahiniwa zaidi ya 500,000 kufanya mtihani kidato cha nne

Mwandishi wetu Timesmajira online

BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA)limesema jumla ya watahimiwa 572,338 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne ambao unatarajia kuanza Novemba 13 hadi Novemba 30 mwaka huu.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es salaam Novemba 12,mwaka huu na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania(NECTA), Dk.Said Mohamed ambapo amesema kati ya watahiniwa hao wa shule ni 543,386 na wakujitegemea ni 28, 952.

Dkt Mohamed amesema watahiniwa hao watafanya mitihani katika shule za sekondari 5,371 na vituo vya kujitegemea 1,798.

“Kati ya watahimiwa wa shule 543,386 waliosajiliwa mwaka huu, wavulana ni 250,237 sawa na asilimia 46.05 na wasichana ni 293,147 sawa na asilimia 53.95,”amesema.

Amesema jumla ya watahiniwa wa shule walio na mahitaji maalumu ni 614 ambao kati yao 283 ni wenye uoni hafifu, 24 ni wasioona, 135 wenye ulemavu wa kusikia ,11 ni wenye ulemavu wa akili na 161 wenye ulemavu wa viungo vya mwili.

Dkt Mohamed alibainisha kuwa mwaka jana, jumla ya watahiniwa wa shule waliosajiliwa walikuwa 534,753 hivyo kuwa na ongezeko la jumla ya watahiniwa 8,633 sawa na asilimia 1.61 kwa mwaka huu ukilinganisha na mwaka jana.

“Kati ya watahiniwa wa kujitegemea 28,952 waliosajiliwa, wavulana ni 11,867 sawa na asilimia 40.99 na wasichana ni 17,085 sawa na asilimia 59.01.

“Watahiniwa wa kujitegemea wenye mahitaji maalumu wako nane , wenye uoni hafifu ni wanne na wasioona ni wanne,”alisema.

Dk.Mohamed ameeleza kuwa jumla ya watahiniwa 10,927 wamesajiliwa kufanya mtihani wa maarifa (QT) ambapo wanaume ni 4,020 sawa na asilimia 36.79 na wanawake ni 6,907 sawa na asilimia 63.21.

Amesema watahimiwa wa maarifa wenye mahitaji maalumu ni 38 ambao wote ni wenye uoni hafifu.

Pia amesema mwaka jana jumla ya watahimiwa waliosajiliwa walikuwa 12,110 hivyo kuwa na upungufu wa jumla ya watahiniwa 1,183 sawa na asilimia 9.77.

Dkt Mohamed amesisitiza kuwa mtihani wa kidato cha nne ni muhimu kwa kuwa hupima umahiri wa wanafunzi katika yale yote waliyojifunza Kwa kipindi cha miaka minne ya elimu ya sekondari yani kidato cha kwanza hadi cha nne.

Aidha ametoa wito kwa kamati za mitihani za mikoa na halmashauri zihakikishe kuwa usalama wa vituo vya mtihani unaimarishwa kwani vituo hivyo vinatumika kwa mujibu wa mwongozo ulioyolewa na NACTE.

Pia aliwataka wasimamizi wote walioteuliwa kusimamia upimaji kufanya kazi yao ya usimamizi kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu.

“Wasimamizi wanapaswa kuhakikisha kuwa, wanafanya kazi ya usimamizi kwa weledi na kwa kuzingatia kanuni za mitihani na miongozo waliyopewa ili kila mwanafunzi husika apate haki yake”amesema