January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wataalamu wa Afya, jamii watakiwa kutoa elimu ya unyonyeshaji watoto

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Daktari bingwa wa watoto kutoka hospitali ya Agakhan, Mariam Noorani
amewataka wataalamu wa afya na jamii kwa ujumla kuungana kwa pamoja katika kutoa elimu kuhusiana na umuhimu wa unyonyeshaji wa watoto kwa ufanisi

Dkt. Noorani ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam kwenye maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji duniani ambapo alisema kwa sasa asilimia 64 pekee ya watoto nchini ndio wanaonyonya maziwa ya mama.

Pia alishauri kufanyika kwa maboresho hususani sehemu za kazi kutenga muda na sehemu maalumu za kunyonyeshea kwa watumishi waliojifungua.

“Unyonyeshaji bora zaidi unaweza kuokoa maisha ya watoto zaidi ya 800,000 kila mwaka, ili kunyonyesha kwa mafanikio akina mama na watoto wachanga wanahitaji usaidizi kutoka kwa familia, jamii, wafanyakazi wa afya na watunga sera. Kwa pamoja tunaweza kutatua changamoto na kuboresha viwango vya unyonyeshaji nchini Tanzania”

“Kwa wiki hiyo huwa wanatumia kama fursa ya kuhamasisha kutoa elimu, kuelekeza, na kushawishi kila mtu kusaidia wakina mama na watoto wanaonyonyesha, ni muhimu kila mtu awe anatoa elimu sahihi hasa kwa wataalamu ili wakina mama waweze kunyonyesha vizuri”

Akielezea umuhimu wa lishe bora kwa mama anayenyonyesha mtaalamu wa lishe kutoka Aga Khan Luiza Tumaini alisema ni muhimu kuzingatia matumizi ya vyakula vinavyoongeza virutubisho muhimu kwa maziwa ya mama ikiwemo matunda mbogamboga na vyakula vyenye protini ili kulinda madini kwenye mwili na maziwa ya mama

“Vyakula ambavyo mama anayenyonyesha anavyotakiwa kula ni vyakula vyenye mbogamboga, na matuta, watu wengi sikuhizi wakishajifungua wanakula vyakula vya vimiminika kama mtori ambapo wanakosa baadhi ya vyakula ambavyo vina virutubisho vizuri kwenye maziwa ya mama”

Kwa upande wake mtaalamu wa lishe na masuala ya unyonyshaji Idda Katigula alisisitiza umuhimu wa utunzaji wa maziwa ya mama kabla ya matumizi huku Afisa ukuzaji Afya njema kutoka kampuni ya bima ya jubilee Milembe, Makoi akisisitiza kuwa kampuni hiyo imeendelea kutoa huduma bora za bima ili kulinda afya ya mama na mtoto.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Huduma za Afya ya Aga Khan, Tanzania (AKHS,T) Sisawo Konteh aliwakumbusha wahudhuriaji na jamii kwa ujumla kwamba kunyonyesha ni kipengele cha msingi cha Afya ya Jamii ambacho kinatoa faida nyingi kwa watoto wachanga na kina mama.

Alisema kama wataalamu wa Afya wataendelea kusaidiana na kuunga mkomo serikali, watoa huduma za Afya, viongozi wa jamii na jamii kwa ujumla kuboresha na kuweka mazingira rafiki ya kunyonyesha katika vituo vyao vyote.

Wiki ya unyonyeshaji duniani huadhimishwa kila Agosti 1 mpaka 8 kila mwaka ambapo kwa mwaka huu imebebwa na kauli mbiu isemayo “kutatua changamoto na kufanikisha unyonyshaji kwa wote duniani”