May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wastaafu watarajiwa Morogoro,Mtwara na Zanzibar wafundwa

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online, Moro

Watumishi wanaotarajiwa kustaafu katika taasisi za serikali na mashirika binafsi wameaswa kuweka mikakati thabiti ya matumizi bora ya rasilimali fedha sambamba na kupata elimu sahihi kuhusu huduma za kifedha na uwekezaji wa miradi sahihi ili waweze kuona matunda ya mafao yao pindi wanapostaafu.

Mwito huo umetolewa na viongozi waandamizi wa Benki ya NBC katika mikoa ya Morogoro, Mtwara na Zanzibar walipopata fursa ya kuzungumza na wastaafu hao watarajiwa kwenye Semina ya siku mbili iliyoandaliwa na mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na kudhaminiwa na wadau mbalimbali ikiwemo benki hiyo.

Akizungumza kwenye moja ya semina hizo mkoani Morogoro, Meneja Mikopo kutoka Benki ya NBC Mtenya Cheya amewaasa watumishi hao kuheshimu na kutunza fedha katika taasisi zinazoaminika sambamba na kubuni vyanzo mbalimbali vya mapato kwa kufuata ushauri madhubuti kutoka kwa wataalamu.

“Benki ya NBC tumejipanga kuwasaidia wastaafu watarajiwa na wale waliokwisha staafu na ndio sababu pamoja na kushiriki kwenye semina za mafunzo kama hizi pia tumekuwa na mikakati na huduma bora kwa wastaafu ikiwemo kutoa mikopo inayozingatia mahitaji yao,’’ alisema.

Akizungumza pia kwenye semina kama hiyo Mkoani Mtwara, Meneja wa benki hiyo tawi la Mtwara Emmanuel Mseti aliwaasa wastaafu hao watarajiwa kuhakikisha wanawashirikisha wataalamu wa fedha pindi wanapofikiria kuhusu mawazo ya biashara, uwekezaji na matumizi sahihi ya mikopo yao ili kujihakikishia ufanisi wa matumizi ya mafao yao.

“Ndio maana benki ya NBC tumekuwa na utaratibu mzuri wa kuwapatia mafunzo wateja wetu kupitia mipango mbalimbali ukiwemo mpango wa Klabu za biashara na utoaji wa mafunzo ya ujasiriamali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kufanya biashara wateja wetu kabla hatujawajakopesha,’’ alisema.

Baadhi ya maofisa wa benki ya NBC tawi la Morogoro wakiongozwa na Meneja wa tawi hilo, Sophia Mwombela (Kulia) wakifuatilia semina ya Watumishi wanaotarajiwa kustaafu katika taasisi za serikali na mashirika binafsi iliyoandaliwa na mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na kudhaminiwa na wadau mbalimbali ikiwemo benki hiyo. Wengine ni Meneja biashara NBC Morogoro, Joseph Boaz (Kushoto) na Meneja mikopo NBC makao makuu, Mtenya Cheya (Katikati).

Wito kama huo pia ulitolewa Zanzibar na Mkuu wa bidhaa na Mauzo wa Benki hiyo, Abel Kaseko ambapo aliwasihi wastaafu hao watarajiwa Zanzibar, kuhakikisha wanahifadhi pesa zao kwenye taasisi rasmi za kifedha ili kuepuka matapeli.

“Zaidi pia tuhakikishe tunaanza uwekezaji mapema ili kujijengea uzoefu utakaotusaidia kujiandaa na maisha ya baadae. Ifahamike kwamba matumizi sahihi ya fedha hizi ndio utakaosaidia wengi wetu kuondokana na utegemezi baada ya kustaafu,’’ alisema.

Pamoja na kuishukuru benki hiyo kwa nasaha hizo muhimu, washiriki wa mafunzo hayo kutoka katika taasisi mbalimbali walielezea namna walivyonufaika na mafunzo hayo huku wakikiri kwamba wengi wao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kushindwa kujiwekea akiba, matumizi yasiyo sahihi ya mafao baada ya kustaafu na kushindwa kubuni mawazo mazuri ya uwekezaji wa fedha hizo.

“Niwashukuru sana watu wa PSSSF kwa kuhusisha wataalamu mbalimbali kwenye semina hizi zikiwemo benki kama NBC kwa kuwa wametufumbua macho kwenye mambo mengi na kwa kweli kupitia elimu hiyo itatusaidia sana,’’ alisema Bw Ali Mselem Ali, mstaafu mtarajiwa kutoka Zanzibar.