Na Mathew Kwembe, Arusha
Timu za Netiboli za JKT Mgulani na Uhamiaji zote kutoka jijini Dar es salaam jana zilipoteza michezo yake ya Ligi daraja la kwanza baada ya kukubali kipigo kutoka kwa TAMISEMI QUEENS ambao ni Mabingwa wa Kombe la Netiboli la Muungano mwaka 2019, katika mchezo mkali na wa kusisimua uliochezwa jana katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid ya jijini Arusha.
Timu ya JKT Mgulani ndiyo ilikuwa ya kwanza kukumbana na kipigo kutoka kwa TAMISEMI QUEENS baada ya kupoteza mchezo wake kwa kufungwa magoli 46-32.Katika mchezo huo uliotawaliwa na ufundi mwingi wa netiboli hadi robo ya kwanza inamalizika TAMISEMI QUEENS walikuwa wanaongoza kwa magoli 18-3.
Katika robo ya pili na ya tatu TAMISEMI QUEENS walikuwa mbele kwa magoli 30-10, na baadaye 40-19 na hadi mchezo unamalizika katika robo ya nne na ya mwisho, TAMISEMI QUEENS walishinda mchezo huo kwa magoli 46-32.
Katika mchezo huo mkali uliochezwa asubuhi, TAMISEMI QUEENS walilazimika kuwapumzisha baadhi ya nyota wake kama vile Sophia Komba, anayecheza eneo la katikati, Golikipa Chuki Kikalao na Mlinzi Mersiana Kizenga kwani timu hiyo ilikuwa na mchezo mwingine mgumu dhidi ya uhamiaji mchana.
Nyota wa mchezo huo alikuwa ni Mshambuliaji wa pembeni wa timu hiyo Lilian Jovin ambaye alionyesha umahiri mkubwa wa kufunga magoli kila mara alipolikaribia goli la JKT Mgulani.Katika mchezo mwingine kati ya TAMISEMI QUEENS dhidi ya Uhamiaji ya Dar es salaam ambao ulichezwa jana jioni katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, hadi mwisho wa mchezo TAMISEMI QUEENS ilifanikiwa kuilaza Uhamiaji magoli 49-31.
Timu zote mbili zilionyesha nia ya kushinda mchezo huo kwani hadi robo ya kwanza ya mchezo inamalizika, timu hizo zilitoka sara kwa kufungana magoli 9-9.Mambo yalibadilika katika robo ya pili na ya tatu kwani wachezaji wa TAMISEMI QUEENS mara kwa mara walikaribia goli la Uhamiaji na kufanikiwa kutumbukiza mipira 23 dhidi ya 14 ya uhamiaji na katika robo ya tatu TAMISEMI QUEENS walifanikiwa kutumbukiza mipira 35 dhidi ya 20 ya Uhamiaji.
Katika robo ya mwisho, wachezaji kutoka timu zote mbili walionekana kuchoka, na hivyo kupunguza kasi ya mchezo huo mkali na wa kusisimua lakini hata hivyo timu ya TAMISEMI QUEENS ilifanikiwa kuongeza magoli mengine baada kumuongeza mchezaji wake mkongwe Aziza Itonye (GA) ambaye mara kwa mara alifanikiwa kufunga mpira kwenye goli la uhamiaji.
Magoli ya TAMISEMI QUEENS katika mchezo dhidi ya Uhamiaji yalifungwa na Lilian Jovin, na Aziza Itonye na kwa upande wa Uhamiaji magoli yalifungwa na Fatuma Machenga na Matalena Mhagama.
Timu hiyo ya TAMISEMI QUEENS ambayo ndiyo timu pekee inayotoka katika Wizara za kiserikali kwa sasa imebakiza michezo miwili ambayo ni dhidi ya Eagles Queens na Mbweni JKT zote za jijini Dar es salaam huku, mchezo wao dhidi ya Mbweni JKT utahitimisha mashindano haya tarehe 29 julai 2021.
Naye, Mwenyekiti wa Klabu ya Michezo ya TAMISEMI Philbert Rwakilomba amesema timu yake imekuja hapa Arusha kupambana ili ibebe kombe la ligi daraja la kwanza mwaka huu.
Amesema, timu yake ilijiandaa vizuri kushiriki mashindano hayo na akawapongeza Viongozi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kuiwezesha timu yake kufanya maandalizi mazuri na hatimaye kushiriki mashindano hayo.
Rwakilomba pia amewapongeza waandaji wa mashindano hayo Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa mapokezi mazuri ambayo timu yake imeyapata na pia amekipongeza Chama cha mchezo wa Netiboli Tanzania CHANETA kwa kusimamia kanuni na taratibu za mashindano hayo.
Kwa upande wake Afisa Michezo wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Benson Maneno ameishukuru CHANETA kwa kukubali mashindano ya Ligi daraja la kwanza Netiboli kufanyika Arusha mwaka huu, na ameahidi kutafuta wadhamini zaidi ili mashindano hayo yatakapofanyika tena Arusha hapo mwakani washindi waweze kupata zawadi nono zaidi.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania