May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waomba kuwekewa alama za kivuko cha watembea kwa miguu

Alama za pundamilia (mistari iliyochorwa barabarani) na picha ya pundamilia ishara inayoashiria kuwa eneo hilo ni kivuko cha watembea kwa miguu.(Picha ya mtandao)

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WANANCHI wa Mtaa wa Hazina Kata ya Hazina jijini Dodoma wameiomba Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Dodoma kurudishia alama za pundamilia (kivuko cha watembea kwa miguu) katika eneo la Hazina mkabala na shule ya msingi Mlezi katika barabara ya Mirembe iendayo mjini na eneo la maghorofa ya TBC mtaa wa Mlezi barabara ya Iringa ili kuwanusuru na kuwalinda dhidi ya ajali hasa watoto wanaosoma katika shule hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wamesema katika barabara hiyo inayopakana na shule ya msingi Mlezi eneo la darajani baa ,kulikuwa na alama za pundamilia ambazo zimefutika muda mrefu  na hivyo kusababisha usumbufu kwa watoto hasa wakati wa kuvuka barabara wakiwa wanakwenda shuleni na  kurudi nyumbani.

Paulina Msonga mkazi wa Mtaa wa Hazina amesema kufutika kwa alama hizo imekuwa changamoto kubwa kwa watoto hasa wale wa darasa la awali ,darasa la kwanza pamoja na wale wenye mahitaji maalum.

Timotheo Francis Mfanyabiashara katika mtaa huo wa darajani baa amesema, ipo haja ya Mamlaka zinazohusika kufanya haraka kuweka michoro hiyo kabla shule hazijafunguliwa ili kuwanusuru na ajali wanafunzi shuleni hapo.

“Tunaiomba Mamlaka husika ilipe uzito suala hili hasa ikizingatiwa shule yetu hii ya Mlezi ina watoto wenye mahitaji maalum lakini pia wapo wale watoto wadogo kabisa ambao kuvuka barabara kwao ni changamoto.”amesema Timotheo

Naye Mhandisi wa Miradi TANROADS Mkoa wa Dodoma Colman Gaston amesema Wakala huo unalifanyia kazi suala hilo .

Kwa mujibu wa tawimu za Shirika la Afya Duniani,ajali za barabarani ni sababu namba moja inayosababisha vifo vya watoto wenye umri wa kati ya miaka hadi 14 na vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 29 ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa.

Pia takwimu hizo zinasema zaidi ya watu miioni 1.35 hufariki kwa ajali za barabarani duniani huku wengine milioni 20 hadi 50 wakiachwa na majeraha na ulemavu wa kudumu.

Katika kuhakikisha watoto wanakua kwa ukamilifu wao,Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali,ilizindua Programua Jumuishi ya Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ya miaka mitano (PJT-MMMAM) 2021/22-2025/26 ili kutatua changamoto za ukuaji na maendeleo ya watoto wenye umri wa miaka sifuri hadi minane ili Taifa lipate nguvu kazi yenye tija hapo baadaye.

Pia wananchi hao wameliomba Jeshi la polisi kuwapa mafunzo ya usalama barabarani wanafunzi wakubwa wanaosoma madarasa ya juu katika shule hiyo ili waweze kuwavusha barabara wanafunzi wenzao hasa wakati wa kwenda shuleni.

“Tunaona kuna baadhi ya shule kama vile Amani shule ya msingi kuna wanafunzi ambao wamepewa mafunzo na muda wa asubuhi huvalia ‘reflector’ wakiwa na vifaa vingine vya usalama barabarani na kusadia kuwavusha wenzao chini ya usaidizi wa Asari Polisi,

“Kwa hiyo na katika eneo letu la magorofa ya TBC Mlezi barabara ya Iringa na eneo la darajani barabara inayotoka hospitali ya Mirembe kuelekea kanisa la Roma,tunaomba kuwepo na wanafunzi hao ili waweze kusaidiana  na Asari Polisi kuwavusha watoto kwa lengo la kuwalinda dhidi ya ajali.”amesema Angelina Mapunda na kuongeza kuwa

Kufuatia ombi hilo  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma  Martin Otieno ametoa maelekezo kwa kitengo kinachohusika  kufanya kazi hiyo huku akisema mara baada ya shule kufunguliwa Januari 2024,suala hilo litafanyiwa  kazi.