May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanyama albino nchini waongezeka

Na Penina Malundo, TimesMajira Online

KAMPUNI ya Tour ya Tanzania Specialist Com imesema kuwa kuna ongezeko la kuonekana kwa wanyama adimu Albino katika kaskazini mwa Tanzania kwenye wiki za hivi karibuni.

Taarifa iliyotolewa juzi jijini Arusha na Muongoza Watalii wa Kampuni hiyo,Joseph Laizer amesema kuonekana kwa wanyama hao Albino kunaonekana kuwavutia watalii wengi kwani wanyama hao uonekana kwa nadra sana.

Akitaja miongoni mwa Wanyama hao ambao ni albino ambao walioonekana ni pamoja na Twiga,Pundamilia katika Mbuga ya Serengeti,pia wapo nyani na nyati maeneo mengine ya nchi kama Ngorongoro na Arusha national Park.

Amesema ni asilimia chache ya wanyama hawa kuonekana kwani inategemea na mahali wanapokuwa.”Ni ajabu sana kuonekana kwa wanyama hawa kwani ni asilimia moja tu ya wanyama ndo wapo wa aina hii hivyo uonekanaji wao ni wanadra sana,”amesema na kuongeza

“Ila kwa siku za hivi karibuni tumekuwa tunashuhudia kuwaona katika mbuga mabalimbali ikiwemo Serengeti, Ngorongoro pamoja na Arusha national Park,hii inawafanya hata watalii wanaokuja nchini kufurahia kuwaona wanyama hao,”amesema.

Aidha amesema wanyama hao wenye ualbino wanakuwa wachache kutokana na mzuko wao wakuzaliana kuwa wa miaka hadi miaka kutokana na vizazi vyao vya miaka ya nyuma.

“Si muda mrefu, watu walishangaa kushuhudia nyati mweupe kabisa ndani Mbuga ya Tarangire na wageni wa mwezi huu walimwona pundamilia mweupe ambaye alikuwa ametoka kuvuka Mto Mara Kaskazini mwa Serengeti.” amesema Laizer

Amesema wataalam wanaripoti kuwa ,sababu kadhaa huchangia kuongezeka kwa kuonekana wanyama albino nchini Tanzania ni kutokana na hali ya ualbino inayoathiri utengenezwaji wa melanini mwilini.

“Melanin ni rangi ambayo hutoa rangi kwa ngozi, macho, nywele, manyoya na makucha kwa wanyama, hali hii ni sawa kwa wanadamu,ambapo Ualbino hutokea kizazi hadi kizazi ambapo kama wazazi wanavina saba vya ualbino,”amesema na kuongeza

“Tunajua kulikuwa na wanyama wa albino miaka 50 au 60 iliyopita lakini kwa kweli, utalii katika miaka ya 1960 haukuwa kama ulivyo leo,kulikuwa na waongoza watalii wachache ambao wengi walikuwa sio wataalam na hata mitandao ya kijamii ilikuwa hamna , kwa hivyo si rahisi kutathmini,”amesema

Amesema vizazi kuanzia hapo hawakuona wanyama wengine wenye ualbino tangu alipoanz kufanya kazi ya kuongoza watalii hadi sasa.

“Kwa vizazi baada ya hapo, hatukuona wanyama wengi wa albino,mimi nilianza kufanya kazi kama mwongozo miaka 15 iliyopita, na ni miaka saba iliyopita ambapo tumeona ongezeko hili.”amesisitiza