May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanne wapoteza maisha kwa ajali ya gari Bukoba

Na Ashura Jumapili, Timesmajira Online,Bukoba,

Watu wanne wamepoteza maisha huku 21 wakijeruhiwa katika ajali iliyohusisha gari lenye usajili namba T 339 DBV aina ya Hiace iliyokuwa ikitokea Izimbya Bukoba Vijijini kuelekea Bukoba Mjini kupinduka maeneo ya Kyetema wilayani Bukoba.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Blasius Chatanda,akizungumza na Waandishi wa Habari katika eneo ambalo ajali ya gari imetokea ameeleza kuwa ajali hiyo imetokea Desemba 5,2023 majira saa tano na nusu asubuhi maeneo ya Kyetema katikati ya Kata mbili za Kemendo na Bujugo Halmashauri ya Bukoba.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Blasius Chatanda akiongea na Wananchi eneo ilipotokea ajali

Kamanda Chatanda,amesema kati ya watu hao waliopoteza maisha katika ajali hiyo watu wazima ni 3 huku mtoto ni mmoja na majeruhi 21 kati yao watoto ni 4 na watu wazima 17 ambao walikimbizwa katika hospitali ya Bujuna Ngoma wilayani humo.

Amesema kutokana majeruhi wengi kuwa na hali mbaya wengine wamehamishiwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera iliopo Bukoba mjini kwa ajili ya kuendelea na matibabu zaidi.

Ameeleza kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva aliokuwa nao wakati akishuka kwenye mteremko mkali.

Ambapo aliweka gari free (Neutro )hivyo alishindwa kuirudisha kwenye mfumo wa gia na kugonga nguzo za umeme zilizokuwa kando ya barabara na pikipiki zilizokuwa kwenye maegesho ya barabara.

“Uzembe wa mtu mmoja unaweza kusababisha waliopata ajali kupata elemavu wa kudumu na kuwa tegemezi katika familia au jamii,”amesema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera.

Hata hivyo Kamanda Chatanda,amewataka madereva wazingatie sheria za usalama barabarani wanapoendesha vyombo vya moto na wakiwa na abiria.

Aidha amesema kuwa hadi sasa haijafahamika kama dereva yuko hai au amefariki amedai kuwa ikithibitika yuko hai sheria itachukua mkondo wake.

Hiece iliyopata ajali na kusababisha vifo vya watu 4 na majeruhi 21 yenye namba ya usajili T 339 DBV eneo la Kyetema

Amesema waliofariki na majeruhi walio wengi bado hawajatambuliwa hivyo amewataka wananchi kufika katika hospitali hizo kutambua ndugu zao.