May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanawake waogopa kugombea wadhfa wakihofia talaka

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online. Zanzibar

IMEELEZWA kuwa tatizo la wanawake wengi kutoshiriki katika vyombo mbalimbali vya maamuzi pamoja na kushika nafasi za uongozi, baadhi yao huogopa kupewa talaka na kuachika kwenye ndoa zao.

Hayo yamesemwa Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja juzi wakati wa mkutano maalumu ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Wanawake (TAMWA-Zanzibar) na kuwashirikisha baadhi ya wawakilishi wa vyama vya siasa na viongozi wa shehia, wenye lengo la kuhamasisha jamii kuwaunga mkono wanawake katika kushiriki kwenye uongozi.

Amewasilisha mada katika mkutano huo, Yumna Mmanga alisema Zanzibar imejaliwa kuwa na neema kubwa ya wanawake wenye uwezo mkubwa na wengine ni wasomi, lakini cha kushangaza hadi sasa wamebaki kuwa mama wa nyumbani, jambo analoamini kuna sababu ikiwemo ya kuhofia kupewa talaka.

Amesema kitendo cha wanawake wengi kuhofia kupewa talaka, bado ni miongoni mwa vikwazo vinavyowakwamisha wanawake wengi na ipo haja jamii kubadilika ili kutoa fursa kwa wanawake.

Yumna amesema huwenda hofu hiyo kwa wanaume, inatokana na baadhi ya wanaume kuwa na uelewa mdogo wakiamini kuwa mwanamke kushiriki kwenye uongozi, huwenda wakadharau waume zao jambo ambalo halina msingi.

Thuwayba Juma Hussein, aliyewahi kugombea nafasi ya Uwakilishi Jimbo la Mahonda kupitia Chama cha ACT-Wazaledo, amesema alipoamua kugombea alikutana na changamoto mbalimbali.

Amesema cha kushangaza zaidi ni watu waliokua karibu yake walimvunja moyo na kumshangaa alipofanya maamuzi hayo, lakini hakurudi nyumba ingawa wengine walimtaka ajitoe.

Thuwayba amesema, kutokana na kujiamini kwake aligombea na wanaume watatu kwenye hatua ya awali ya kutafuta uteuzi wa chama, ambapo alifanikiwa kuwa mshindi wa mwanzo na chama chake pia kumrudisha kuwa mgombea.

Kwa upande wake, Ali Sleiman ambaye ni Katibu wa Shehiya Sheha ya Mkokotoni amesema katika shehia yake kuna wanawake ambao wamepewa nafasi kuwa kwenye Kamati za Shehiya na wanafanya kazi zao vizuri.

Amesema kwa uwajibikaji wa wajumbe hao, ambao ni wanawake kwenye kamati hiyo ni wazi kwamba wanawake wengi, wakipewa nafasi kumbe wana uwezo mkubwa kiutendaji.

‘’Sikuwa nikifahamu awali kama wanawake wana uwezo kiasi kile kwenye kazi, niliamini wanawake ni watu wasiokua na uwezo kabisa,’’ amesema.

Naye Katibu wa Baraza la Vijana Wilaya ya Kaskazini A Unguja, Fatma Sharif Ibrahim amesema awali katika shehiya ya Kipange wakati anateuliwa Sheha mwanamke jamii, ilimdharau na kuelewa wazi wazi kuwa hataweza kuongoza shehia hio.

Amesema licha ya kusemwa kwake vibaya, lakini mwanamke huyo hakukata tamaa na alifanya kazi zake kwa weledi mkubwa na hadi sasa amekua kivutio kwa walio wengi.

Fatma amesema changamoto nyingine ni mifumo ya vyama vya siasa kupitia katiba zao, bado hakujawekwa fursa sawa za kikatiba ambazo zingeweza kuwabeba wanawake.

Amesema kwenye vyama vyote vya sasa Tanzania, bado katiba zao hazijaweka wazi kutoa fursa za upendeleo kwa wanawake wanatakaoshindana na wanaume kwenye kura za awali.