May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanaotaka kuihujumu CCM Hanag kukiona

Na Jumbe Ismailly, TimesMajira Online, Hanang

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Hanang, Mkoani Manyara kimewatahadharisha baadhi ya viongozi wanaofanya vikao usiku vya kukihujuma chama hicho na kuweka wazi kwamba hakitasita kuwachukulia hatua za kisheria kwa kufanya vikao vyao bila kuwa na vibali.

Mkuu wa Wilaya ya Hanang ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya siasa ya Wilaya hiyo, Ghaib Lingo ametoa tahadhari hiyo kwenye mkutano wa hadhara wa kuwatambulisha wagombea wateule wa ubunge na udiwani uliofanyika kwenye viwanja vya michezo vya Kijiji cha Endasaki.

Amesema kuwa, uchunguzi uliofanywa na vyombo vya dola umebaini kwamba kuna baadhi ya viongozi wa kata tano za wilaya ya Hanang wanaojihusisha na vikao vya usiku huku wakitambua kuwa kwa kufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi.

Kwa mujibu wa Lingo ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, amesema baadhi ya viongozi hao baada ya majina ya wagombea wao kutoteuliwa na vikao vya juu, wameanza kukaa na wanachama kwenye maeneo yao na kuwashawishi kukinyima kura Chama Cha Mapinduzi na badala yake wapigie kambi ya upinzani.

“Nina kata tano ambazo viongozi wa chama wanafanya kazi hizo usiku nilikuwa nafikiri siku nikiamka vibaya niwashike niwaweke ndani kwa sababu kufanya mikutano usiku bila kibali cha polisi ni kosa, mimi nitashindwa kukutungia kesi wewe kwani hata leo tumepata kibali cha polisi ndiyo tunakutana hapa, ” amesema kiongozi huyo.

Hata hivyo Lingo ameweka bayana kuwa, baada ya wagombea wateule wa kiti cha ubunge na udiwani kutambulishwa kwa wanachama na wananchi kwa ujumla aliwaomba kuwachagua viongozi walioteuliwa na chama hicho ili waweze kuwaletea maendeleo endelevu.

Kikundi cha kwaya kutoka Kata ya Endasaki kikitumbuiza wananchi na wanachama wa CCM waliohudhuria hafla ya kuwatambulisha wagombea wateule wa nafasi za Ubunge na udiwani.

Mkuu wa wilaya huyo amesisitiza kwamba ili wananchi wa Hanang wasiweze kumlaumu mwakilishi wao wa ubunge kwamba ameshindwa kutekeleza masuala la maendeleo, hawana budi kuhakikisha wanawachagua wagombea wateule wote waliopendekezwa na chama hicho.

Aidha Lingo ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya siasa ya chama hicho amesema ifikapo Oktoba 28 mwaka huu, wanachama wa chama hicho na wananchi wa Hanang kwa ujumla wahakikishe kura za kishindo zinakwenda kwa mgombea wa kiti cha urais, wabunge na madiwani ili kukamilisha mafiga matatu yanakamilika.

“Maana ya mafiga matatu ni kwamba kuwachagua wagombea wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),kwa kutoa kura nyingi na za kishindo kwa Rais,wabunge na kwa madiwani kwani ukiondoa figa moja mambo hayatakwenda sawasawa maana hata unapopika chakula chungu kitakaa vizuri kwenye mafiga hayo yote” amefafanua Mkuu wa wilaya huyo.

Akiwatambulisha wagombea wateule wa ubunge na udiwani wapatao 33, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Hanang, Mathew Dalema amesema, baada ya wagombea hao kuteuliwa na vikao vya juu vyenye mamlaka ya kufanya hivyo, hivi sasa kazi iliyobakia kwao ni kuwanadi kwa wapigakura ili waweze kushinda kwa kupata kura za kishindo.

“Baada ya wagombea kuteuliwa na vikao vya juu vyenye mamlaka ya kufanya hivyo hivi sasa kazi iliyobakia kwetu ni kuwanadi kwa wapigakura ili wagombea wetu waweze kushinda kwa kupata kura za kishindo, ” amesisitiza Mwenyekiti huyo wa CCM.

Baadhi ya madiwani wateule wa viti maalumu wakijinadi kwenye mkutano wa hadhara wa kuwatambulisha wagombea wateule wa Ubunge na Udiwani wa wilaya ya Hanang,Mkoani Manyara.

Kwa upande wake aliyeongoza katika kura za maoni za ubunge, George Bajuta ametumia mkutano wa kuwatambulisha wateule kukanusha taarifa zilizozagaa kwamba baada ya kutoteuliwa ameamua kuhama CCM na kujiunga na vyama vya upinzani.

“Kuna baadhi ya watu ndani na nje ya chama wanaozusha kwamba Bajuta anahama chama,waambieni wanikome,kwani nimekulia ndani ya ccm,nimelelewa na ccm na nitafia ccm hivyo wale wote wenye mawazo hayo watukome na waniache na ccm yangu.”alifafanuaBajuta.

Akizungumza na wanachama pamoja nawananchi wa Kata ya Endasaki, mgombea ubunge mteule, Hhayuma Samweli Xabay amewahakikishia kuwa endapo watampa ridhaa ya kuwa mwakilishi wao atashirikiana nao kumaliza migogoro iliyopo kati ya wakulima na wafugaji.,

“Migogoro ni mingi, ikiwemo ya wakulima na wafugaji na nia yangu ni kushirikiana nanyi tuweke mpango mkakati mzuri wa matumizi yetu ya ardhi ya Hanang, lakini pia na tarafa yetu ya Endasaki.”amesisitiza mgmbea huyo.