May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanaofoji nembo ya TBS kwenye bidhaa waonywa

Na Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Rukwa

Shirika la viwango Tanzania TBS limesema halitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria ikiwemo kuwapiga faini ya shilling million 20 wajasiliamali na wasindikaji watakao bainika kufoji nembo ya TBS pamoja na kuingiza sokoni bidhaa zisizokuwa na ubora.

Hayo yamebainishwa na kaimu meneja wa shirika la viwango Tanzania Tbs kanda ya Magharibi Rodney Alananga wakati akitoa elimu kwa wajasiliamali, wasindikaji na wamiliki wa viwanda na kufanyika katika ofisi za kata ya Matai wilayani Kalambo mkoani Rukwa,Ambapo amewataka waandaji wa bidhaa kuzingatia weledi na viwango na ubora wakati wa uandaaji wa bidhaa kabla ya kuingizwa sokoni.

‘’Tbs inazo skimu mbalimbali za udhibiti ubora ikiwemo skimu ya alama ya ubora,mzalishaji ambaye bidhaa yake imethibitishwa ubora kwa kuzingatia kiwango cha kitaifa cha bidhaa husika hupewa leseni ya kutumia alama ya TBS katika bidhaa hiyo hivyo kwa mwaka 2024 mzalishaji yeyote ambaye atashindwa kuwa na alama hiyo kwenye bidhaa yake atazuiliwa bidhaa yake kuingizwa kwenye maonesho makubwa ikiwemo nane nane na saba saba. Amesema. – Alananga.

Alananga amedai kuwa katika ulimwengu wa kisasa biashara ni ushindani hivyo ukitaka kuingia huko ni vizuri kuhakikisha bidhaa zinazalishwa kitaalamu na kufuata kanuni na kubwa ni la bidhaa kuwa nembo ya ubora ya TBS.

Amedai kuwa kutokana na ushindani huo kuna baadhi ya wazalishaji na wasindikaji wa bidhaa kwa kukosa weredi wamekua wakifoji nembo ya TBS ili kuendana na mazingira ya soko na kuwa kufanya hivyo ni kosa kubwa la kisheria na atakayebainika akifanya hivyo atachukuliwa hatua kali kwa mjibu wa sheria na hakuna atakayeachwa salama katika hilo.

Wazalishaji na Wasindikaji wa bidhaa hizo kwa upande wao wamesema kuwa kwa kipindi kirefu wamekuwa wakitengeneza bidhaa zao bila ya kuzingatia ubora na kuwa sasa toka shirika hilo lianze kutoa elimu hiyo wengi wamefahamu na kuwa katika kipindi cha mwaka ujao wa 2024 hakuna mzalishaji au msindikaji ambaye ataendelea kuzalisha bidhaa bila ya kuzingatia kanuni za ubora.

Julius Kapele amesema kuwa bidhaa bora zinawalinda wateja wao na kuwa kama watalizingatia hilo bidhaa zao ni rahisi kuvuka hata mipaka na kuuzwa kimataifa na kuweza kujiongezea kipato.

Shirika la viwango Nchini kanda ya Magharibi limekuwa likikutana na watu wa kada mbalimbali wakiwemo wazalishaji na wasindikaji bidhaa katika kuwaelimisha namna ya kutengeneza bidhaa zenye ubora na kuhakikisha kuwa bidhaa zao zinakua na Nembo ya TBS ikiwa ni pamoja na kuweleza mchakato wa upatikanaji wa nembo hiyo.

Kaimu meneja wa TBS kanda ya magharibi Rodney Alananga akitoa mafunzo kwa wazalishaji na wasindikaji wa bidhaa mbalimbali mkoani Rukwa