June 1, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi wamzomea Meneja RUWASA Songwe

Na Moses Ng’wat, Momba.

MENEJA wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mkoa wa Songwe, Mhandisi Charles Pambe, amezomewa na wananchi wa Kijiji cha Naming’ongo, Wilayani Momba katika mkutano wa hadhara baada ya kuonesha kutoaridhishwa na maelezo juu mikakati ya upatikanaji maji katika eneo hilo.

Wakazi hao walimzomea Meneja huyo baada ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, kumtaka atoe majibu kuhusu kero ya upatikana wa maji kufuatia mmoja wa wa wakazi hao kuwasilisha kero ya ukosefu wa maji katika mkutano huo wa hadhara uliofanyika Mei 16, 2024 katika kijiji hicho cha Naming’ongo, ikiwa ni siku ya mwisho ya ziara ya kikazi ya Mkuu wa Mkoa katika Wilaya hiyo iliyolenga kukagua miradi ya maendeleo na kufanya mikutano ya hadhara.

Wakati Meneja huyo akiendelea kutoa majibu, ikiwemo kuainisha mikakati mbalimbali ya Ruwasa ya kumaliza kero ya ukosefu wa maji katika Kijijini hicho.

Ghafla zilianza kusikika kelele za kuzomea kutoka kwa wananchi hao zikienda sanjari na maneno, anakudamganya, anakudanganya,anakudanganya.

Hali hiyo ilimshtua Mkuu wa Mkoa ambapo alimsimamisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Kenani Kihongosi, huku akiwatuliza wananchi.

“Sikilizeni, sikilizeni…sasa hivi hawadananyi ninyi, ananidanganya mimi, sasa sikilizeni Mkuu wa Wilaya hebu sogea pale na umemsikia huyu jamaa (Meneja Ruwasa), baada ya Wiki mbili (Juni 5, mwaka huu), wewe Mkuu wa Wilaya ukiongozana na huyu bwana njooni mfungue maji kwenye hicho kisima anachosema,tumeelewan, sasa ole wako maji yasitoke na wananchi siku hiyo ikifika saa tatu asubuhi nendeni pale Zahanati kwenye hicho kisima mkangalie kama hayo maji yanatoka au hayatoki na mkiona mambo sio basi mimi nina namna yangu ya kupata taarifa nitakuja haraka” alihitimisha chongolo hali iliyoibua shangwe kubwa kwa wananchi.

Awali akieleza mikakati ya Ruwasa katika kuwafikishia maji wanachi hao kabla ya kukatizwa na zomea zomea ya wakazi hao, alisema katika kijiji hicho Ruwasa imepeleka mradi mkubwa wa maji utakaogharimu shilingi bilioni 7.2 na unatarajia kuhudumia vijiji 8 katika kata mbili za Chitete na Msangano.

Aliongeza kuwa, kwa kutambua kuwa mradi huo mkubwa utachelewa, wakala huo uliamua kuwachimbia kisima wakazi hao wa Kijiji cha Naming’ongo ambapo uchimbaji huo utakamilika baada ya wiki mbili.