Joyce Kasiki,Msomera Handeni
MSOMERA KUMENOGA’ ndivyo wanavyosema wananchi walioanza kuishi kijiji cha Msomera miaka mingi iliyopita pamoja na wale waliohama kwa hiari kutoka hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro mkoani Arusha na kuhamishiwa kijiji cha Msomera wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Msomera sasa ni kijiji kinachong”ara kwa nyumba nzuri na bora zilizojengwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambalo ndio limepewa kazi ya kujenga nyumba za kuishi wananchi wanaohama kwa hiari kutoka Hifadhi hiyo ya Ngorongoro.
Kijiji hicho kilichokuwa pori la akiba sasa kimepambwa na nyumba hizo nzuri pamoja na miundombinu mbalimbali ya huduma za kijamii zikiwemo barabara zinazotoka eneo moja hadi eneo jingine na hivyo kukifanya kijiji hicho kuvutia.
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT ) kupitia shirika lake la Uzalishaji Mali (SUMAJKT) ndiyo wanaofanya kazi ya ujenzi wa nyumba hizo pamoja na miundombinu ya elimu ,afya na barabara kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali kwa lengo la kuhakikisha huduma zote za kijamii zinapatikana katika vijiji vya Msomera na Saunyi mkoani Tanga na kijiji cha Kitwai mkoani Manyara wanavyohamia wakazi hao.
Mkuu wa Tawi la Utawala JKT ambaye pia ndiye Kamanda Kikosi ujenzi wa nyumba 5000 Brigedia Jenerali Hassan Mabena anasema Ujenzi wa nyumba hizo 5000 ni awamu ya pili huku akisema awamu ya kwanza JKT lilipewa jukumu la kujenga nyumba 402 ambazo zilishakamilika na watanzania waliokubali kuhama kwa hiari kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro kwenda katika eneo hilo walishahamia na tayari wanaendelea na maisha.
Wajiweka sawa kujenga nyumba bora na kwa wakatiÂ
Brigedia Jenerali Mabena anasema baada ya kupewa jukumu hilo ,JKT lilikaa chini na kutafakari namna ya kutekeleza mradi huo kwa haraka na kwa ubora madhubuti lakini kwa gharama nafuu na likaona namna nzuri ya ujenzi iwe ni katika mpango wa oparesheni ambapo Maafisa na Askari wa Jeshi la wananchi wa Tanzania, watumishi wa umma na vijana wa JKT wanashiriki katika ujenzi huo.
“Lakini pamoja na kutumia rasilimali watu hiyo ,vifaa pamoja na mitambo, magari ambayo yanamilikiwa na SUMAJKT pamoja na vikosi vya Jeshi la Kujenga Taifa yaliratibiwa vyema na kupelekwa eneo la ujenzi tayari kwa kazi “anasema Brigedia Jenerali Mabena
Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Mabena ,kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kisekta kama vile Wakala wa Barabara za mijini na vijijini (TARURA), maji ,umeme na mawasiliano wamefanya kazi kubwa ya kuhakikisha miundombinu yote inajengwa na kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii.
Aidha anasema ili kuleta nafuu katika ujenzi wa nyumba hizo vifaa kama vile milango,madirisha na matofari vinazalishwa na JKTÂ huku akisema ujenzi huo unahusisha vikosi vyote vya JKT vilivyopo hapa nchini.
Anasema licha ya kuwepo changamoto ya mvua nyingi zilizoharibu miundombinu ikiwemo ya barabara na kukatika kwa umeme mara kwa mara lakini Jeshi lilitatua changamoto hizo kwa kununua majenereta  ambayo yalikuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa njia tatu kutokana na mashine wanazotumia kutumia umeme mkubwa.
Kwa mujibu wa Kamanda Kikosi huyo,hatua hiyo ilirahisisha kazi na hivyo kwenda kwa haraka na kasi inayotakiwa na kuwawezesha kujenga nyumba 2559 tangu walipofika na kuanza kazi hiyo ya ujenzi kwa kujiandaa mazingira  katika kijiji cha Msomera ambapo mpaka sasa tayari nyumba 1000 zimekamiia na nyumba 1559 zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Waliotoka Ngorongoro wafurahia ,wampongeza Rais Samia
Wananchi waliohamishiwa katika kijiji hicho kutoka hifadhi ya Ngorongoro wameonesha kufurahishwa na nyumba hizo ambazo ni nzuri lakini pia na namna kijiji hicho kilivyopangwa vizuri .
Sailep Supokumelea ni miongoni mwa wananchi hao ambaye anasema amehama Ngorongoro kwa hiari yake huku akifurahia uhuru wa kumiliki mali tofauti na walivyokuwa wakiishi Ngorongoro.
“Naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan,kweli aliona mbali ,maana mimi tangu nimekuja huku Msomera najiona ni tofauti sana na nilivyokuwa Ngorongoro,nimekuwa na uhalali wa kumiliki Mali wakati kule tulikuwa haturusiwi hata kuwa na pikipiki tu,
“Lakini huku ukiacha nyumba niliyojengewa na Serikali ambayo pia nimepewa na hati kabisa,nimejenga na mjengo wangu,yaani Serikali imefanya vizuri kutuhamishia Msomera na wale wengine ambao bado wapo Ngorongoro waje Msomera kuchangamkia fursa hii ya Serikali,nawaambia waje huku Msomera kumenoga.”anasema Sailep
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Msomera Martine Ole Ikayo ambaye ni mzaliwa wa kijiji hicho naye amempongeza Rais Samia na serikali kwa ujumla kwa kuwafanya wananchi waliohamia Msomera kutoka Ngorongoro kuwa na maisha mazuri.
“Waliohamia kutoka Ngorogoro wameshauwa na maisha mazuri,mashamba yamestawi na mifugo yao inaendelea vizuri,Serikali imeweka miundombinu ya barabara, umeme,maji ,lakini bado inaendelea kuleta maji kutoka mto Pangani kwa lengo la kupunguza ama kuondoa kabisa changamoto ya maji ,mawasiliano ilikuwa ni changamoto kubwa lakini sasa tuna minara miwili.”anasema Ole Ikayo
Miundombinu ya Elimu na afya nayo yajengwa
Vile vile mwenyekiti huyo anasema tayari Serikali kupitia JKT imejenga miundombinu ya elimu ambapo kuna shule mbili zimejengwa ikiwemo ya Dkt.Isdory Philip Mpango ambayo ni ya mtaala mpya yenye darasa la awali hadi kidato cha nne na shule ya msingi ya Samia Suluhu Hassan pamoa na miundombinu ya afya na tayari imeshaanza kutoa huduma kwa wananchi.
Ametoa wito kwa wananchi ambao bado wapo Ngorongoro waende Msomera wakaboreshe maisha yao ikiwa ni pamoja na kufanya shughuli nyingi za kiuchumi na kumiliki Mali ikiwemo nyumba na mashamba.
Ametumia nafasi hiyo kwa kupongeza ujenzi unaofanywa na JKT huku akisema Jeshi hilo linafanya kazi usiku na mchana ili kuharakisha ukamilishaji wa nyumba walizokabidhiwa kuwezesha zoezi la wananchi kuendelea kutoka hifadhi ya Ngorongoro.
Mwalimu Mkuu shule ya mfano iliyojengwa kwa mpango wa mtaala mpya kwa maana ya kutoka darasa la awali mpaka kidato cha nne Ibrahim Mhina anasema shule hiyo imependekezwa jina la Dkt.Isdory Philip Mpango huku akisema zoezi la kuandikisha wanafunzi hasa wale waliotoka Ngorongoro linaenda vizuri kwani mwitikio ni mkubwa.
Florah Ortumo Mkazi wa kitongoji cha Tembo kijiji cha Msomera ameishukuru serikali kwa huduma za afya elimu na maji pamoja na kujenga miundombinu yote muhimu inayowawafanya wajivunie kuishi katika kijiji cha Msomera.
“Mimi nimefurahi kuona miundombinu mingi imejengwa hasa ya elimu maana watoto wangu wote kule Ngorongoro waliwakuwa wanasoma,mwanzoni nilipokuja nikaona shule hakuna nikaanza kusikitika lakini tunashukuru Serikali tunaona maendeleo yanakuja ,kama hivi mnavyoona tayari shule imejengwa ,
“Maisha ya Ngorongoro na huku Msomera ni tofauti sana,kule mtu alikuwa hana hata kiwanja anachomiliki mwenyewe lakini hapa nina kiwanja changu na nyumba,nina hati,nina shamba napanda mazao nakula vizuri ,kwa hiyo naona huku ni kuzuri zaidi kuliko Ngorongoro.”anasema Florah
Martine Singoya Mwenyeiti wa Kitongoji cha Mkababu kijiji cha Msomera ambaye pia ni mzaliwa wa eneo hilo anasema kabla ya uhamisho  wa wananchi wa Ngorongoro kwenda Msomera walikuwa wanapata shida na waliishi katika mazingira magumu kutokana na kukosekana kwa miundombinu mbalimbali na huduma za kijamii.
Anasema lakini baada ya wananchi kuanza kuhamia kutoka Ngorongoro kijiji kimekuwa na maendeleo makubwa kwani miundombinu mingi imeboreshwa na mingine imejengwa upya kama vile ya elimu ,afya ,barabara ,mawasiliano,maji na afya .“Kama hivi mnaona shule imejengwa nzuri ,ni shule ya mfano maana sidhani kama kuna sehemu imeengwa shule kama hii ,tuna maji barabara nyingi kiasi cha wenzetu wanakwenda Dar es Salaam wakirudi hapa kijijini huwa wanapotea kwani pamekuwa ni mji mzuri wenye barabara nyingi sana,lakini tuna maeneo ya kunyweshea mifugo yetu tofauti na zamani tulikuwa tunatembea umbali wa kilomita 18 kutafuta maji kwa ajili ya kunywesha mifugo.”
“Mimi kama mwenyekiti wa kitongoji cha Mkababu nawaambia wananchi waliobaki Ngorongoro watoke huko na waje Msomera kumenoga kupo vizuri sana na tunasema asante sana Rais Samia kwa sababu kama hawa wenzetu wasingekuja huenda tusingeweza kupata mradi mubwa huu .”anasema Singoya
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best