May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi wahofia mtuhimiwa kuachiwa kwa dhamana

Na Lubango Mleka, TimeMajira Online,Igunga

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Mbutu, Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora wameliomba Jeshi la Polisi wilayani hapa kufanya uchunguzi wa kina kwa mtuhumiwa Masanja Bukwimba (43) mkazi wa Kijiji cha Mbutu, Kata ya Mbutu ambaye ni Mtuhumiwa namba moja kati ya watuhumiwa watatu wanaotuhumiwa kutaka kumuua Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga Mussa Abdallah (38) kwa kumkata na kitu chenye ncha kali shingoni Machi 10, 2023 mtaa wa Mwayunge.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kijijini hapo na waandishi wa habari, baadhi ya wananchi hao waliojitambulisha kwa majina ya Kizengele Nkwanda, Jihogo Mwanambulu na Mkiwa Jilonga wamesema kuwa wao hawaingilii sheria za Mahakama kwa kuwa dhamana ni haki ya mtu yoyote anapokidhi vigezo vya dhamana.

Wamesema kuwa, wameamua kupaza sauti zao katika vyombo vya habari ili mamlaka za juu ziweze kujua kwa undani kwani mtuhumiwa huyo Masanja alishafanya mauaji sehemu mbalimbali hapa nchini kwa kukodiwa na baadhi ya watu mbalimbali.

Wananchi hao wameyataja baadhi ya maeneo aliyowahi kufanya mauaji kwa kuwakata mapanga kuwa ni pamoja na Mkoa wa Dodoma, Wilaya ya Bahi ambako anatuhumiwa kuuwa watu wawili, mwanamke na mwanaume ambapo alikamatwa na kukaa katika gereza la Isanga lilipo Mkoa wa Dodoma kwa miaka miwili kisha kutoka na kurudi Igunga.

Sehemu nyingine ni Mkoa wa Morogoro, Singida Wilaya ya Kiomboi, Ikungi, Tabora Wilaya ya Uyui, kijiji cha Tura na Wilaya ya Igunga kijiji cha Makomero ambako anatuhumiwa kufanya mauaji kwa mkulima kwa kumkata mapanga.Aidha wananchi hao wamebainisha kuwa hayo ni baadhi ya maeneo aliyofanya unyama huo na kusema kuwa hata Polisi wilayani hapa wanajua vizuri juu ya matukio ya mtuhumiwa huyo ambapo kwenye vitabu vyao zipo kumbukumbu zake.

“Ndugu zangu waandishi wa habari, mkitaka kujua vizuri muulizeni hata Inspekta Edward kwani anajua vizuri sana wakati alikuwa hajahamishwa kwenda Tabora Mjini kikazi, huyo Masanja alitoweka Igunga kwa kuwa alikuwa anamsaka ili amfikishe kwenye vyombo vya sheria.” amesema Mwanambulu.

Sambamba na hayo wananchi wamesema kwa sasa wanaishi kwa hofu sana na ndiyo maana wameliomba Jeshi la Polisi Igunga lifanye uchunguzi wa haraka dhidi ya mtuhumiwa huyo na ikiwezekana wafanye mawasiliano katika maeneo yote aliyowahi kufanya uhalifu.

Diwani wa Kata ya Mbutu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga Lucas Bugota amesema yeye hawezi kuzungumzia kwa kirefu tuhuma za mtuhumiwa Masanja.

“Mimi siwezi kuzungumzia sana mambo ya Masanja lakini ana mambo ya kona kona, pia mtu huyo ni hatari sana na ndiyo maana sikuweza kwenda kumuona Polisi au Mahakamani,”amesema Bugota.

Amebainisha kuwa, baada ya kusikia amekamatwa wananchi wake walikuwa na amani sana lakini waliposikia ametoka kwa dhamana hivi sasa yeye na wananchi wake wanaishi bila amani huku akisema wananchi wake wamekuwa wakijiuliza kila anapokamatwa amekuwa akitoka bila kujua kinachoendelea.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora Kamishna Msaidizi, Richard Abwao amesema endapo wananchi wanazo taarifa zenye ushahidi mzuri wa matukio ya uhalifu yaliyofanywa na Masanja Bukwimba katika baadhi ya maeneo hapa nchini waende kwa viongozi wa kituo cha Polisi Igunga wakatoe taarifa ambapo Jeshi la Polisi litafuatilia kwa haraka.

Hata hivyo, Kamanda Abwao amewatoa hofu wananchi wa Kata ya Mbutu na maeneo mengine kuwa Jeshi la polisi liko imara kwa kuimarisha ulinzi katika maeneo yote.

Itakumbukwa kuwa hivi karibuni Jeshi la Polisi Wilaya ya Igunga lilifanikiwa kuwakamata watu watatu wakiwemo watumishi wawili wa Igunga, Jahulula Edward Jahulula (41) aliyekuwa Kaimu Ofisa Ardhi Igunga ambaye kwa sasa amehamishiwa Wilaya ya Bariadi Mkoa wa Simiyu.

Emmanuel Ikandiro (48) Mhandisi Halmashauri ya Igunga na kuwafikisha Mahakama ya Wilaya ya Igunga wote watatu wakikabiliwa na shitaka moja la kutaka kumuua Mussa Abdallah (38) kwa kumkata na kitu chenye ncha kali shingoni ambapo wote wapo nje kwa dhamana ya milioni 3 kila mmoja.