Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Korogwe
IMEELEZWA kuwa baadhi ya wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wameshindwa kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa (ICHF) sababu hawana uhakika wa kupata dawa pindi wanapokwenda kwenye vituo vya afya.
Hayo yalisemwa Mei 12, 2022 kwenye Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, ambapo hadi robo tatu ya mwaka wa fedha 2021/2022, ni asilimia 6.4 ya wananchi ndiyo wamejiunga na ICHF katika halmashauri hiyo.
“Moja ya sababu iliyofanya wananchi kushindwa kujiunga na Bima ya Afya ya ICHF ambayo imeboreshwa ni kukosa dawa wanapokwenda kwenye vituo vya afya, kwani wanaambiwa dawa hakuna, hivyo wanalazimika kwenda nje kununua dawa kwa fedha zao.
“Tunaamini changamoto hii ya dawa imefika mwisho baada ya Serikali kufumua mfumo mzima wa MSD (Bohari Kuu ya Dawa) baada ya kuona kuna mambo yanayokwamisha wananchi kupata dawa” alisema Mwenyekiti wa Huduma za Jamii ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Lutindi Emmanuel Mng’ong’ose wakati anajibu maswali ya madiwani.
Ni baada ya Diwani wa Kata ya Makuyuni Richard Mndolwa kuhoji ni kitu gani kinakwamisha wananchi kujiunga na ICHF, na nini kifanyike ili kuweza kuwasaidia wananchi kujiunga na bima hiyo.
Diwani wa Viti Maalumu Tarafa ya Mombo Agness Mapanda alisema ipo haja ya kuwa na magari ya kubeba wagonjwa (Ambulance) ya kutosha, kwani wamechoka kuona wanawake wajawazito wakibebwa na bodaboda kupelekwa vituo vya afya.
“Tumechoka kuona wanawake wajawazito wakibebwa na bodaboda kwenda kwenye vituo vya afya. Sasa tunataka kujua ni lini Serikali itanunua ambulance ili kuweza kubeba wanawake wajawazito hasa waliopo vijijini kuwapeleka vituo vya afya pindi wakiwa na changamoto mbalimbali” alisema Mapanda.
Diwani wa Viti Maalumu Tarafa ya Magoma, Mwanaisha Gogo alisema wanawake wanaojifungulia Zahanati ya Mashewa wanadhalilika, kwani wanajifungulia kwenye jengo dogo ambalo ndani yake kuna huduma nyingine, ambapo wakati mwanamke huyo anapiga kelele ya uchungu, wanaume na watoto wanamsikia.
“Jengo la Mama, Baba na Mtoto. Sehemu ya kujifungulia haliridhishi. Ni sehemu ndogo, hata mama akiwa anajifungua anadhalilika kila anapolalamika kwa uchungu wa kujifungua, wanamsikia watoto na wababa. Tunaomba bajeti ipangwe kujengwe leba ili kuondoa udhalilishaji kwa wanawake” alisema Gogo.
Mng’ong’ose alisema shida wanayopata wanawake wanaojifungua kwenye Zahanati ya Mashewa ni kwa sababu jengo lililopo liliungua moto miaka mitatu iliyopita, hivyo jitihada mbalimbali zinafanyika ili kupata fedha na kujenga jengo ambalo litakidhi huduma kwa Mama, Baba na Mtoto, huku akieleza namna watakavyonunua magari ya wagonjwa.
“Suala la kujenga jengo la Mama, Baba na Mtoto linafanyiwa kazi. Mbunge wetu wa Jimbo la Korogwe Vijijini Timotheo Mnzava analifanyia kazi kuona tunapata fedha ili liweze kujengwa. Lakini pia na ofisi yako Mwenyekiti inalifanyia kazi jambo hili. Kuhusu kununua magari ya wagonjwa, hilo tunatakiwa kuongeza mapato kwenye vyanzo vyetu vya Mapato ya Ndani. Tunaamini tutafanikiwa” alisema Mng’ong’ose.
Bima ya Afya ya ICHF iliyoboreshwa, inaiwezesha kaya ya watu sita, yaani mke, mume na watoto wanne kupata matibabu kwa mwaka mzima kwa kulipa sh. 30,000.
More Stories
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari