May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi 9,659 kunufaika na mradi wa maji malungu Nyasa

Na Mwandishi Wetu , Timesmajira Online,Ruvuma

Mradi wa maji Malungu unaotekelezwa kwa gharama ya bilioni 1.2, unatarajiwa kuwanufaisha wananchi 9,659,kutoka vijiji vya Malungu na Tingi vilivyopo katika Kata ya Tingi wilayani Nyasa.

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nyasa Mhandisi Masoud Samila,amesema mradi utasaidia kupunguza magonjwa mbalimbali ya mlipuko kwa jamii.

Meneja huyo amebainisha hayo Machi 17,2024 wakati akitoa taarifa ya utekelezaji ya mradi huo katika muendelezo wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira ya kukagua utekelezaji wa miradi ya Maji mkoani Ruvuma.

“Kutokana na kuimarika kwa huduma ya maji, jamii itapata muda wa kufanya shughuli za maendeleo,”amesema Mhandisi Samila.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Jackson Kiswaga ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa usimamizi na utekelezaji wa miradi.

“Mradi huu ukamilike kwa wakati pia wananchi muweze kutunza miundombinu yake ili iwe endelevu lakini chombo cha watumiaji maji katika jamii kiundwe ili kiweze kukusanya fedha na kufanya matumizi mazuri ya ukarabati wa mradi pindi inapotokea umeharibika,”amesema Kiswaga.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amemuagiza Meneja wa RUWASA Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshonga, kuhakikisha anapeleka huduma ya maji kwenye vitongoji ambavyo havina maji.

Pia Mhandisi Mahundi ametoa rai kwa wananchi kuendelea kutunza vyanzo vya maji ili miradi ya maji iwe endelevu.