December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi 4,164 kunufaika na mradi wa maji Mnyuzi

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Korogwe

WANANCHI wa baadhi ya vijiji vya Kata ya Mnyuzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wapatao 4,164 watanufaika na Mradi wa Maji Lusanga , na kuondoa adha ya wananchi hao kuliwa na mamba Mto Pangani.

Hayo yalisemwa Juni 2, 2022 na Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Korogwe Mhandisi William Tupa wakati anasoma taarifa ya mradi huo kwa Kiongoxi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahili Geraruma.

Tupa alisema RUWASA imetekeleza Mradi wa Maji Lusanga kwa fedha za Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF), ambapo utekelezaji wa mradi huo ulianza Aprili 15, 2019 na ulikamilika Juni 16, 2021, ambapo sh. milioni 682,495,870 zimetumika katika kutekeleza mradi huo.

“Lengo la mradi huu ni kutekeleza adhma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuondoa kero ya maji kwa wananchi wapatao 4,164 kwa vijiji vya Lusanga, Shambakapori, Ngomeni na Shule ya Sekondari Mnyuzi. Na kazi zilizopangwa na kutekelezwa katika mradi huu ni pamoja na ujenzi wa tanki la ujazo wa lita 90,000 katika Kijiji cha Lusanga, ujenzi wa tanki la ujazo wa lita 45,000 katika Kijiji cha Ngomeni.

“Ujenzi wa tanki la ujazo wa lita 23,000 katika Kijiji cha Shambakapori, ujenzi wa tanki la ujazo wa lita 23,000 Shule ya Sekondari Mnyuzi, ujenzi wa vituo 20 vya kuchotea maji (vilula), ujenzi wa nyumba ya mtambo wa kusukumia maji (Pump House), ujenzi wa Ofisi ya Watumiaji Maji (CBWSO), uchimbaji wa mtaro na kufunga bomba kuu (Rising Main) mita 8,326” alisema Mhandisi Tupa.

Mhandisi Tupa alisema kazi nyingine ni uchimbaji wa mtaro na kufunga mabomba madogo madogo (Distribution Network) mita 10,828, na kufunga pampu na vifaa vya nishati ya umeme..

Alisema ili mradi huo uwe endelevu, wananchi wameshirikishwa katika hatua zote za utekelezaji wa mradi. Aidha katika michango ya wananchi, wameweza kutoa maeneo yao ambayo yametumika kujenga miundombinu ya maji.

Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini mkoani Tanga Timotheo Mnzava alisema wananchi wa Kijiji cha Lusanga walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya maji, na kulazimika kuchota maji Mto Pangani ambapo walikuwa wanahatarisha maisha yao kwa kuliwa na mamba.

Mnzava alisema Kijiji cha Lusanga hakina shule ya msingi, lakini sasa inajengwa, na madarasa matatu yamejengwa na yapo usawa wa boma, na Mfuko wa Jimbo umetoa mabati 120 kwa ajili ya kupaua, huku Serikali ikitoa sh. milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa darasa jingine la nne.

Mnzava alisema pia Kijiji cha Lusanga kilikuwa hakina umeme, lakini sasa kina umeme, na jitihada zinafanyika kusambaza umeme kwenye vitongoji, na barabara inayoingia kwenye kijiji hicho imetengenezwa.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Geraruma alisema ameridhishwa na kazi iliyofanywa na RUWASA, huku akimmwagia sifa Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo kwa kazi kubwa na nzuri aliyofanya.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Kalisti Lazaro akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni Siriel Mchembe, alisema miradi itakayotembelewa na Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ni saba na ina thamani ya sh. bilioni 3.19.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahili Geraruma (kulia) akimtwisha ndoo mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Lusanga, Kata ya Mnyuzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe. Ni baada ya kufungua Mradi wa Maji Lusanga. (Picha na Yusuph Mussa).
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahili Geraruma (katikati) akifungua Mradi wa Maji Lusanga uliopo Kijiji cha Lusanga, Kata ya Mnyuzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe. Wengine ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Kalisti Lazaro (kushoto) na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Korogwe Vijijini Nassoro Malingumu (kulia). (Picha na Yusuph Mussa).
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Mhandisi William Tupa akisoma taarifa ya Mradi wa Maji Lusanga mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahili Geraruma, kwenye Kijiji cha Lusanga, Kata ya Mnyuzi. (Picha na Yusuph Mussa).
Moja ya vilula (DP) vilivyopo Kijiji cha Lusanga, Kata ya Mnyuzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe.. (Picha na Yusuph Mussa).
Nyumba ya mtambo wa kusukumia maji (Pump House) iliyopo kwenye Mradi wa Maji Lusanga Kijiji cha Lusanga, Kata ya Mnyuzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe. (Picha na Yusuph Mussa).