May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DMO awataka Maofisa Ustawi kuwatembelea watu wa kuaminika katika jamii(Fit Person)

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Imeelezwa kuwa watu wa kuaminika katika jamii (fit person) ni muhimu katika malezi ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu,hivyo wito umetolewa kwa Maofisa Ustawi wa Jamii kuwatembelee ili kutambua changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi.

Wito huo umetolewa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Dkt. Sebastian Pima wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo watu wa kuaminika katika jamii(fit person) waliopo katika Halmashauri hiyo ambayo yamefadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la SOS Children’s Village na kufanyika jijini hapa.

Ambapo amewahimiza Maofisa ustawi kuwatembelee watu wa kuaminika katika jamii ili kutambua changamoto zinazowakabili wakati wa kulea watoto wanaowapelekea.

Huku akiwapongeza watu wa kuaminika katika jamii kwa kujitolea kuwahudumia watoto ambao wamekuwa na changamoto mbali huku akiwataka kuwahudumia na kuwalea watoto wanaopelekewa kama watoto wao.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Edith Mokiwa,amebainisha namna ambavyo ofisi yake inashirikiana na watu wa kuaminika katika malezi ya watoto wanaopata changamoto katika familia zao.

Ambapo amesema,kwa Halmashauri hiyo imeishapata watu wa kuaminika 48 na katika mafunzo hayo jumla ya watu 20 wameshiriki ili kuwakumbusha katika masuala mazima ya malezi kwa watoto hao.

Amesema,wanawapeleka watoto ambao ni yatima na wametelekezwa na ndugu pamoja na wale waliokinzana na sheria kabla ya kumrejesha kwao anapitia mafunzo kutoka kwa watu wa kuaminika ili akawe mtoto mwema.

“Watu wa kuaminika ni watu wetu muhimu sana, kwenye sheria ya mtoto,inaelekeza kuwa mtoto anapaswa kuwa kwenye familia na siyo kwenye taasisi ndio maana ikaanzishwa watu wa kuaminika na kweli watu hawa wametusaidia sana tunachangamoto ya watoto wengi kupoteza kwa sababu wanakuja kwenye Jiji la Mwanza Kanda ya Ziwa hapa ndio mji mkubwa kwaio watoto wengi wanakuja na tunapata watoto wengi sana mfano katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022, jumla ya watoto 103 tumewapa watu wa kuaminika,”ameeleza Mokiwa.

Meneja Miradi wa shirika la SOS Children’s Village kwa Mkoa wa Mwanza Dorothy Ndege, amesema watu hao ni muhimu sana kuwa nao kwenye jamii kwa sababu wanasaidia kupokea watoto kutoka sehemu mbalimbali kutokana na changamoto ambazo wamepitia pia inawarahisishia malezi kwa watoto wanaowapojea kwenye makao yao.

“Tunaamini sehemu salama ya mtoto kuishi ni nyumbani kwenye familia na kwenye makao iwe ni uamuzi wa mwisho ndio maana tunahamasisha hawa watu wa kuaminika wawepo wake na watoto hao kwa muda usiozidi miezi sita wakati mchakato wa kutafuta familia yake ukiendelea,”amesema Ndege.

Mratibu wa Malezi Mbadala kutoka shirika la SOS Children’s Village kwa Mkoa wa Mwanza Anthony Mkinga, ameeleza kuwa wameamua kufadhili mafunzo hayo kutokana na umuhimu wa watu wa kuaminika katika jamii kwani kumekuwa na changamoto nyingi za watoto wengine wanapotea na kutupwa.

Hivyo kabla ya watoto hao kufikishwa katika makao ya shirika hilo ni muhimu hao watu wa kuaminika wawe wanakaa nao wakati Maofisa wakifuatilia wazazi wao halisi au kwenye makao.

Kwa upande wake mmoja wa watu wa kuaminika walioshiriki mafunzo hayo,Cornel Francis amesema changamoto wanayoipata wakati wa kulea watoto hao ni kutokuwa wakweli kwa kila mara kutaka majina tofauti tofauti.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Dkt.Sebastian Pima, akizungumza wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo watu wa kuaminika 20 kutoka kata mbalimbali katika Halmashauri hiyo yaliyofadhikiwa na shirika la SOS Children’s Village yalitofanyika jijini hapa.(Picha na Judith Ferdinand)
Meneja Miradi wa shirika la SOS Children’s Village Dorothy Ndege, akizungumza na timesmajira mara baada ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo watu wa kuaminika katika jamii 20 kutoka kata mbalimbali katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza hiyo yaliyofadhiliwa na shirika hilo yalitofanyika jijini hapa.(Picha na Judith Ferdinand)
Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Edith Mokiwa akizungumza na timesmajira mara baada ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo watu wa kuaminika katika jamii 20 kutoka kata mbalimbali katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza hiyo yaliyofadhiliwa na shirika la SOS Children’s Village yalitofanyika jijini hapa.(Picha na Judith Ferdinand)
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Dkt.Sebastian Pima akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya kuwajengea uwezo watu wa kuaminika katika jamii 20 kutoka kata mbalimbali katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza hiyo yaliyofadhiliwa na shirika la SOS Children’s Village yalitofanyika jijini hapa.(Picha na Judith Ferdinand)