January 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanahabari waingia hofu vifungu vya sheria ‘vitanzi’

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

WAANDISHI wa habari nchini, wameeleza hofu yao kutokana na kifungu cha 35, 36, 50 (1)(a)(ii) kueleza kwamba, kosa la kashfa ni jinai.

Vifungu hivyo vilivyopo katika Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari 2016, vimeelekeza kosa la kashfa kuwa jinai badala ya madai.

Maregesi Paul, Mhariri wa Tanzania Daima katika semina ya wanahabari, jijini Dar es Salaam amesema, kipengele hiki kinalenga kukomoa wanahabari kwa kuwa, uzito wake ni mkubwa tofauti na kosa la kashfa.

“Kosa la kashfa halina uzito mkubwa kama linapogeuzwa kuwa jinai, na walipoliweka hilo ni kwamba wanataka kukomoa. Sasa hapo mwandishi anachukuliwa kama muhujumu uchumi, hii ni hatari sana,” amesema Maregesi.

Regina Mkonde kutoka Mwanahalisi Digital amesema, kosa la kashfa kugeuzwa jinai kunamuweka mwandishi katika hatari zaidi na kumjaza hofu.

Akieleza ufafanuzi wa vifungu hivyo kwa wana habari, mtoa mada James Marenga ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa MISA – TAN pia Wakili wa Kujitegemea amesema, hatua ya kosa la kashfa kugeuzwa jinai, inaongeza hofu na sintofahamu kwa wanahabari nchini.

“Vifungu vya 35, 36, 50(1)(a)(ii) vinafanya kosa la kashfa kuwa ni kosa la jinai badala ya kuwa ni kosa la madai. Tunapendekeza kuwa, mashauri yote yatakayotokana na kashfa yaendeshwe kama kesi za madai sio jinai,” ameeleza Marenga.

Amesema, madhumuni ni kuhakikisha vikwazo katika uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza vinaondolewa.

Mwanasheria huyo amesema, kugeuza kashfa kuwa ya jinai kunaleta hofu na kufifisha haki ya kujieleza na kutoa maoni.

“Kifungu cha 37 kinasema kwamba, uchapishaji wa kashfa ni kosa la jinai isipokuwa kama jambo lililochapishwa ni la kweli na limechapishwa kwa manufaa ya umma; pia kama uchapishaji huo umetolewa kama upendeleo wa kutoshitakiwa (privileged) kwa kashfa na ulikuwa ni manufaa kwa umma,” amesema.

Amesema, kama uchapishaji huo umetolewa kama upendeleo wa kutoshitakiwa (privileged) kwa kashfa na ulikuwa ni manufaa kwa umma, kifungu hicho cha sheria hakijaweka vigezo vingine vinavyoonesha kuwa uchapishaji wa kashfa sio kosa la jinai.