Na Mwandishi Wetu
BENKI ya CRDB imeahidi kuwapa mikopo yenye masharti nafuu na riba ndogo wamiliki wa shule binafsi ambao ni wanachama wa Chama cha Wawekezaji Binafsi katika Elimu (TAPIE).
Ahadi hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa benki hiyo, Abdulmajid Nsekela, wakati akifungua mkutano mkuu wa tatu wa TAPIE Mbezi jijini Dar es Salaam, ambapo yeye alikuwa mgeni rasmi.
Nsekela ametoa ahadi hiyo baada ya kusikia kilio cha wanachama wa chama hicho kuhusu ugumu wnaoupata kupata mikopo na ombi lao la kupungiziwa riba wanapopata mikopo hiyo.
“Ila kutakuwa na masharti madogo na nafuu kama vile mwenye shule kufungua akaunti CRDB na wanafunzi wenu wote kufungua akaunti kwetu maana hawo ni wateja wetu wa baadaye,” amesema Nsekela.
Amewataka wamiliki wa shule binafsi nchini kuwafundisha elimu ya kutunza fedha wanafunzi tangu wakiwa wadogo ili waje kuwa wajasiriamali wakubwa na mahiri wanapomaliza masomo yao ya elimu ya juu.
“Huwezi kuwa mjasiriamali mzuri kama hujui kutunza fedha, sasa wafundisheni umuhimu wa kutunza fedha na wafungulieni akaunti hii itawajengea utamaduni mzuri wakiwa wakubwa ,” amesema Abdulumajid
Pia amepongeza shule binafsi kwa kuendelea kufanya vizuri kitaaluma na aliipongeza pia serikali akisema kuwa kufanya vizuri kwa sekta binafsi katika elimu ni matokeo ya jitihada za serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa sekta hiyo.
Amesema kufanya vizuri kwa shule nyingi binafsi kumewavutia wazazi wengi kuwapeleka watoto wao kwenye shule hizo hata pale wanapofaulu kujiunga na shule mbalimbali za umma.
Amesema kwa kutambua umuhimu wa elimu benki ya CRDB imeiweka sekta ya elimu kama sekta ya kipaumbele kwa kuendelea kuiwezesha kwa mikopo na mitaji.
Nsekela amesema mwaka jana na nusu ya mwaka huu shule nyingi zilipata shida kutokana na janga la COVID 19 lakini benki hiyo iliweka mazingira rafiki kwa kuhakikisha wenye shule wanapewa muda mwingi wa kulipa mikopo.
“Shule nyingi zilikuwa kwenye mapumziko kutokana na janga hilo hivyo hali ya uchumi haikuwa nzuri kwao lakini sisi tuliwapitia mmoja baada ya mwingine kuangalia changamoto yake na kutafuta suluhu,” amesema
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAPIE, Mahmoud Mringo aliomba benki mbalimbali zipunguze riba ya mikopo ili kuwawezesha wamiliki wa shule kupata mikopo nafuu.
Amesema uwekezaji kwenye elimu unachukua muda mrefu kurejesha faida lakini wamekuwa wakipata vikwazo sana kwenye kupata mikopo ikiwemo viwango vikubwa vya riba.
Amesema shule binafsi zimekuwa zikitozwa tozo mbalimbali za serikali hivyo kuwa na mzigo mkubwa wa kujiendesha hali inayowafanya wenye shule wengi kuishi wakiwa na msongo wa mawazo.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi