Na Penina Malundo, Timesmajira Online
WANACHAMA na Wafuasi wa Chama Cha ACT-Wazalendo wa Micheweni kisiwani Pemba wameamua kumchangia fedha Maalim Seif Sharif Hamad kuwania tena urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.
Akizungumza kwa niaba ya Wanachama hao ambao wamemchangia Maalim Seif kiasi cha Sh. 500,000, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Micheweni kichama , Rashid Khalid amesema, wameamua kufanya hivyo kwakua kiongozi huyo ndiye pekee atakayeweza kutetea maslahi ya Wazanzibari .
Amesema kuwa, Wazanzibar wanahitaji muungano na kuwakomboa katika dimbwi la umasikini na ukosefu wa ajira ambavyo vyama vingine vimeshindwa kuwatimizia.
“Tumeamua kukuchangia fedha hizi ili zikusaidie katika kulipia ada ya uchukuaji wa fomu, sisi wanachama wa Micheweni tunaona wewe ndiye mtu pekee utakayeweza kutuokoa kutokana na madhila wanayotufanyia vyama vingine ,” amesema kiongozi huyo.
Baada ya kupokea fedha hizo, Maalim Seif amesema, kiqasi hicho kitamsaidia kupunguza gharama za ada ya uchukuaji wa fomu ya kugombea urais wa Zanzibar ambayo ni shilingi milioni moja.
“Nawashukuru sana kwa mchango huu mlionipa, hii inaonesha mapenzi makubwa mliyonayo kwangu na mimi nasema tena kama nilivyoahidi huko nyuma, nitaendeea kuwatumikia Wazanzibari hadi pale Mwenyezi Mungu atakapochukua uhai wake” amesema Maalim Seif.
Pia amewashukuru wanachama hao na kusema kuwa uongozi wa Chama Cha ACT-Wazalendo kimejipanga vyema katika kuhakikisha kinapata ushindi ili kiweze kuwahudumia wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa kwa wananchi wote.
Julai 4, 2020 Maalim Seif anatarajia kuchukua fomu rasmi ya kuomba kuteuliwa na chama chake ili kugombea nafasi ya urais wa Zanzibar kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2020.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja