Na Fresha Kinasa, Mara
SERIKALI Mkoani Mara imewataka Wakuu wa Shule za Sekondari zote mkoani humo kusimamia suala la nidhamu katika shule wanazozisimamia ikiwemo kudhibiti tabia za baadhi ya Walimu kujihusisha kimapenzi na wanafunzi jambo ambalo limetajwa kuwepo na kuwa sababu mojawapo ya kudhoofisha maendeleo ya elimu mkoani humo.
Imesema kuwa,walimu wanapaswa kutumia dhamana waliyopewa na Serikali kusimamia ubora wa elimu shuleni, pamoja na kuhakikisha kwamba ufaulu katika shule zao unakuwa mzuri katika kuzalisha wasomi wa viwango watakao lisukuma mbele Taifa hivyo rungu zito la adhabu litatua kwa wenye tabia hiyo.
Kauli hiyo imetokewa na Katibu Tawala Mkoa wa Mara Caroline Muthapula Kupitia hotuba yake iliyosomwa na Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Mara Elisonguo Mshiru Wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA), Mkoa wa Mara unaofanyika kwa siku mbili katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songe Girls iliyopo Mjini Musoma Mkoa wa Mara kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujadili masuala mbalimbali ya kuinua Elimu Mkoani humo.
Amesema Kuwa yapo baadhi ya mashauri wamekuwa wakipokea ya Walimu kudaiwa kujihusisha kimapenzi na Wanafunzi, Jambo ambalo amesema Walimu Wakuu wanapaswa kuhakikisha wanasimamia nidhamu kwa Walimu na Wanafunzi ili tabia hiyo isiwepo katika kuhakikisha kwamba ubora wa elimu unasimamiwa kwa ufanisi Mkoani humo.
“Wakuu wa Shule hakikisheni kabisa Walimu hawajihusishi kimapenzi na Wanafunzi, Ni aibu kubwa kuona Mwalimu aliyepewa dhamana kulea watoto kwa kuwafundisha waweze kufauru katika masomo yao halafu anajiingiza kwenye mapenzi na Mwanafunzi, hii inarudisha nyuma ufanisi wa kitaaluma na Serikali haitasita kuchukua hatua Kali kwa watakao bainika kufanya hivyo kufanya mchezo huo mchafu,” amesema.
Katika hatua nyingine,Muthapula amewataka Walimu Wakuu wote wa Shule za Sekondari Mkoani humo kuhakikisha wanashiriki kwa uaminifu na kikamilifu katika mtihani wa moko utakaofanyika Agosti 17, mwaka huu , na kuupa uzito mtihani huo kwa kujiepusha na uvujishaji ikiwa ni njia mojawapo ya kujiandaa kufanya vizuri katika mitihani ya Kitaifa ili kuuondoa Mkoa katika nafasi za Mwisho na uweze kufanya vizuri tofauti na mwaka Jana.
Kwa upande Wake Mwenyekiti wa (TAHOSSA) Mkoa wa Mara Mwalimu Mugisha Galibona amepongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuimarisha sekta ya elimu ikiwemo kukarabati Shule kongwe zilizopo Mkoa wa Mara na nchini nzima, kuongezea miundombinu ya mabweni na Maabara katika baadhi ya shule, pamoja na kutoa mishahara kwa Walimu wote wa Serikali kwa kipindi ambacho Shule zilifungwa kutokana na Janga la Corona.
Naye Katibu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT),Mkoa wa Mara, Lucy Masegenya,amesema mbali na kusisitiza walimu kuzingatia maadili na nidhamu kwa kujiepusha na mapenzi na Wanafunzi, amewaasa walimu kuweka utaratibu wa kutunza kumbukumbu zao ikiwemo barua ya kuthibitishwa kazini, barua ya ajira na vielelezo vyote vya msingi jambo ambalo litawasaidia katika kufuatilia mafao yao wanapokaribia kustaafu.
More Stories
Baraza la wazee Kata ya Kilimani laahidi kampeni nyumba kwa nyumba
TMDA:Toeni taarifa za ufuatiliaji usalama wa vifaa tiba ,vitendanishi
The Desk & Chair yashusha neema Gereza la Butimba