April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof.Joyce Ndalichako

Walimu 352 wapandishwa madaraja Songea

Na Cresensia Kapinga,TimesMajira,Online Songea.

MJUMBE wa Kamati Tendaji Taifa wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Sabina Lipukila amewataka walimu kufanya kazi kwa weredi, kwani mafanikio ya nchi hii yapo mikononi mwao na kwamba kazi hiyo pia imebarikiwa na Mungu licha ya changamoto wanazokabiliana nazo.

Hayo ameyasema jana wakati wa hafla fupi ya kuwakabidhi barua za kupanda madaraja walimu 352 kutoka halmashauri ya Wilaya ya Songea vijijini Mkoani Ruvuma iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.

Amesema Serikali yao ni sikivu imesikia kilio chao cha muda mrefu cha kupandishwa madaraja ili kuwajengea msingi mzuri wa kuendelea kuipenda kazi yao na si vinginevyo.

“Zoezi hili ni uthibitisho huu utumike kama misingi ya kiimani na motisha ya kweli kutoka kwa Rais ambaye aliagiza watumishi waliokaa kwa muda mrefu wapandishwe madaraja, kwani kufanya hivyo kunawapa walimu hawa molari ya kufanya kazikwa bidii,” amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Ruvuma, Kalimeji Sandari aliwapongeza walimu kwa hatua ya kupanda madaraja lakini pia amewashukuru kwa kuwa mstari wa mbele wa kutekeleza majukumu yao licha ya changamoto walizonazo.

“Chama kimeendelea kupigania haki na maslahi kwa wananchama wao na kufanya majadaliano na mwajiri namna ya kupandishwa madaraja bila kutumia nguvu wala maandamano hii imeendelea kuleta mafanikio kwa chama, ambapo kwa mwaka jana Serikali ilipunguza baadhi ya makato kwa walimu na mwaka huu walimu 119,887 wamepandishwa madaraja nchi nzima.”amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Songea Vijijini, Simon Bulenganija amesema ualimu ni wito hivyo aliwataka walimu hao kufanya kazi kwa weredi mkubwa kwa kuzingatia misingi, kanuni, taratibu na sheria za kazi zinavyowataka.

Amesisitiza kwamba Serikali inaendelea kuboresha mazingira yao ya kazi kwa kuwajengea nyumba za walimu.

Walimu hao wameipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kuwapandisha madaraja walimu kutokana na hali hiyo inawapa motisha ya kufanya kazi kwa bidii tofauti na hapo awali.

Wamemshukuru wameshukuru Rais wa awamu ya sita kwa kuwajali na wameomba aendelee na moyo huo wa kuwapandisha madaraja ili kuinua kiwango cha elimu nchini.