January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Walengwa TASAF wasomesha watoto hadi elimu ya juu

Na Reuben Kagaruki, TimesMajira, Online Hai

MPANGO wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umefanikiwa kutimiza ndoto za watoto wengi wanaotoka kwenye kaya hizo baada ya walengwa kujengewa uwezo na hatimaye kuanzisha miradi midogo midogo inayowawezesha kusomesha watoto wao hadi vyuo vya kati na vyuo vikuu nchini.

Ushuhuda huo umetolewa kwa nyakati tofauti na walengwa wa Mpango wa TASAF mkoani Kilimanjaro waliotembelewa na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kwenye makazi yao na kujionea jinsi wanavyoshiriki kupambana na umaskini na kujiimarisha kiuchumi.

Akizungumza na wahariri hao nyumbani kwake, Mtaa wa Kingereka, Kata Bondeni wilayani Hai, mkoani Kilimajaro leo mmoja wa walengwa wa mpango huo, Grace Mkie, amesema wakati mume wake anafariki, watoto walikuwa wadogo na kwamba peke yake bila TASAF ingekuwa kuwafikisha kiwango cha elimu walichopo sasa.

“Baada ya mume wangu kufariki maisha yalikuwa magumu, chakula cheti ilikuwa ni mlo mmoja tena wa usiku,” amesema Mkie. Amesema wakati giza limetanda machoni mwake kuhusiana na namna ya kuwalea watoto hao, ndipo alipoambiwa kwamba kaya yake inastahili kuingizwa kwenye Mpango wa TASAF.

Kwa mujibu wa Mkie, baada ya kuingizwa kwenye mpango huo na kupatiwa fedha za ruzuku, alianzisha mradi wa kufuga kuku na kuuza mayai na kwamba fedha alizokuwa akipata zilimwezesha kusomesha watoto wake wawili waliokuwa sekondari na mmoja shule ya msingi.

“Kile nilichopewa na TASAF nilikieleza kwenye mradi wa ufugaji kuku. Mradi huo uliniwezesha kusomesha watoto wangu,”amesema. Amefafanua kwamba mtoto wake wa kwanza baada kufaulu kidato cha nne, alichaguliwa kujiunga na Chuo cha Mipango mkoani Mwanza na kuanza masomo ya ngazi ya cheti.

Amefafanua kwamba aliweza kumsomesha mtoto wake hadi diploma ya kwanza na alipomaliza aliendelea na diploma ya pili ambapo sasa tayari amemaliza na anaendelea na masomo ngazi ya shahada.

“Mtoto huyu amefika hapo kwa sababu ha TASAF na sasa hivi anapata mkopo,” amesema Mkie na kuongeza anapata mkopo wa asilimia 80 na pengine mkopo ungekuwa zaidi ya hapo, kwani wakati anajaza fomu za mikopo, hakuza kwamba yeye ni mnufaika wa TASAF.

Mwanaasha Mtei, akiwa na watoto wake kwenye nyumba anayojenga kutokana na biashara ndogo ndogo anazofanya baada ya kujengewa uwezo na TASAF. Mbali na kujenga nyumba anasomesha watoto ambapo mkubwa amejiunga na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT)

Aidha, Mkie amesema aliweza kusomesha mtoto wake wa pili hadi akafaulu kidato cha nne na sasa anasoma mwaka wa pili Chuo cha Uhasibu Njiro,jijini Arusha.

Kuhusu mtoto wake wa mwisho, Mkie amesema amehitimu kidato cha nne na amechaguliwa kuendelea na masomo ya ngazi ya cheti na kwamba anakusanya nguvu ili naye aweze kuanza masoko.

“Kwa kweli nasema TASAF wamenisaidia sana, kwani kabla ya wao tulikuwa tunakula mlo mmoja, lakini sasa nimeweza kusomesha watoto wangu hadi vyuo,” amesema na kuongeza; ” Sina cha kusema zaidi ya kuishukuru TASAF na Serikali kwa kuanzisha huu mpango.”

Kwa upange wake, Mkazi wa Kijiji cha Rundugai, Kata Masama wilayani Hai,mkoani Kilimanjaro, Maliwadha Mkumbwa, amesema kabla ya kuingizwa kwenye Mpango wa TASAF maisha yake yalikuwa ya chini na watoto wake walikuwa wanafukuzwa shule kila siku kwa kukosa sale na hakuwa na uwezo wa kuchangia chakula kwa ajili ya watoto shuleni.

Mmoja wa walengwa wa TASAF akiwa kwenye biashara zake. Seforoza Joseph, Kupitia biashara hiyo ameweza kusomesha watoto wake bila vikwazo kama alivyokuwa akikumbana navyo mwanza.

Ametoa ushuhuda kwamba wakati anaingizwa kwenye mpango wa TASAF, watoto wake walikuwa darasa la kwanza, darasa la nne na la saba na kila siku changamoto za kurudishwa nyumbani kwa kukosa mahitaji ya shule ilikuwa sehemu ya kawaida ya maisha yao.

“Baada ya kuingizwa kwenye mpango wa TASAF nilitumia fedha nilizopewa kuanzisha biashara ndogo ndogo, sasa hivi watoto wangu hawarudishwi nyumbani, nimeweza kuwasomesha hadi wameingia vyuoni,”amesema Mkumbwa na kuongeza kwamba mtoto wake wa kwanza anasoma chuo cha VETA Tanga.

Amesema amewafikisha watoto wake kwenye kiwango hicho cha elimu baada ya fedha alizopewa kuzitumia kuanzisha mradi wa kufuga kuku na mbuzi miradi hiyo ndiyo ilihitimisha watoto wake kufukuzwa shule ya msingi kwa kukosa mahitaji.

Naye, Mwanaasha Mtei, anasema Mpango wa TASAF umemsaidia kwenye maisha yake, kwani mwenza wake alimtelekeza baada ya kujifungua watoto mapacha. Mwanaasha mkazi mkazi wa Kijiji cha Rundugai, anasema baada ya kuingizwa kwenye mpango wa TASAF, fedha alizopewa alinunua mbuzi saba na kufuga kuku na alivyokuwa akivuna (kuuza), fedha alizopata zilimsaidia kusomesha watoto.

“Nilipokuwa nikivuna (kuuza) kuku na mbuzi, nilichokuwa nikipata nilikitumia kwa chakula na kujiwekea akiba ambayo imeniwezesha kumpeleka mtoto wangu Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) baada ya kufaulu kidato cha nne,”anasema Mtei na kuongeza kwamba ameweza kulipa mahitaji yote yaliyokuwa yakihitajika kiasi cha sh. 800,000 kuwezesha mtoto kujiunga na chuo kwa masomo ya ngazi ya cheti.

Kwa sasa anasema anachopambana nacho kwa sasa ni fedha za kula na hosteli.