November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima 792 wapewa elimu kuhusu majani mabichi ya chai

Na Mwandishi wetu , Timesmajira Online,Rungwe WAKULIMA 792 wa zao la chai Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya wamehitimu mafunzo ya mwaka mmoja ya shamba darasa yenye lengo la kuboresha kilimo hicho pamoja na kuwawezesha kuchuma majani mabichi ya chai yenye ubora na kuingiza sokoni.

Ofisa Mradi Mwandamizi wa shirika la IDH ,Michael Joseph akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa shamba darasa kwa wakulima 792 kutoka Halmashauri ya Busokelo na Rungwe Mkoa wa Mbeya

Wakulima hao wamenufaika na elimu ya shamba darasa kupitia Taasisi ya Agri Connect Boresha chai inayotekelezwa na shirika lisilo la kiserikali la IDH kwa ufadhiri wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU).

Ofisa Mradi Mwandamizi kutoka shirika la IDH, Michael Joseph akizungumza Agosti 29, mwaka huu kwenye mahafali ya kwanza ya wakulima wadogo 792 walionufaika na mafunzo ya shamba darasa kutoka Halmashauri za Busokelo na Rungwe Mkoa wa Mbeya.

Katika mafunzo hayo ya shamba darasa wakulima wamekaa miezi 12 kwa ajili ya kupata elimu na yamehusisha vikundi 25 ambavyo vimejifunza kwa vitendo.

“Lengo kuu ni kuwajengea uwezo wakulima kuzalisha majani mabichi ya chai yaliyo na tija sambamba na kujikita katika mazao mbadala ya masuala ya lishe bora,utekelezaji wa mradi huo ni wa kipindi cha miaka minne umelenga kuwafikia wakulima wadogo 10,000,”amesema Joseph.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe ,Ally Said amelipongeza shirika hilo kwa kuwafikia wakulima wadogo wa chai na kuwapatia elimu ya uchumaji wa majani mabichi ya chai kupitia shamba darasa.

Amesema kama serikali wana kila sababu ya kuwasaidia wakulima wadogo kuona ni namna gani wanaondokana na changamoto sambamba na kushirikiana na wadau wa shirika la IDH.

“Tumepoke taarifa ya wakulima wadogo wa chai zaidi 792 wamenufaika na elimu ya shamba darasa hivyo niwatake kuwa mabalozi wakubwa wa kutoa elimu hiyo kwa makundi mengine ya wakulima wakati serikali ikiendelea na mpango wa kutatua changamoto za upatikanaji wa vifaa,”amesema Said.

Baadhi ya wakulima wa chai wakicheza kwenye Mahafali ya mwaka mmoja ya shamba dara yaliotolewa na shirika la IDH kwa ufadhiri wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya

Naye Mwenyekiti wa wakulima wadogo wa chai, Issa Mwanyumba amesema tangu kuanza kwa mradi huo wa mwaka mmoja wakulima wameweza kuongeza tija ya uzalishaji wa majani mabichi ya chai mpaka kufikia wastani wa kilo milioni 23 kwa mwaka.

“Ni namna gani elimu iliyotolewa na shirika la IDH ilivyoleta tija kubwa kwa wakulima na matarajio yetu uzalishaji itaendelea kuongezeka kwa kasi na kuchochea kipato cha mkulima mmoja mmoja au vikundi,”amesema.

Amefafanua kuwa kwa miaka ya nyuma wakulima wamejikuta wakishindwa kuendeleza mashamba ya chai kutokana na changamoto mbalimbali ikiwepo uhaba wa pembejeo za kilimo kwa wakati ambapo ujio wa mradi huo umekuwa fursa kwao kuzalisha kwa tija na kuchuma majani yenye ubora.

Kwa upande wake mmoja wa wanufaika wa mradi wa shamba darasa, Maria Mwakanyamale akisoma risala ya wakulima hao amesema changamoto kubwa inayowakabili ni ukosefu wa vifaa kama ,visu mashine ya kuchuma majani mabichi jambo ambalo linakwamisha uzalishaji.