May 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hifadhi ya kitulo kutangazwa kimataifa kuvutia watalii, wawekezaji

Na Mwandishi wetu, timesmajira

Serikali imeendelea kujizatiti kwa kuitangaza Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ndani na nje ya nchi lengo likiwa ni kuwavutia watalii na wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali Duniani kupitia maonesho, matamasha na kwa njia ya kidijitali.

Kauli hiyo imesemwa leo Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Makete, Festo Sanga aliyetaka kujua mkakati wa Serikali wa kuitangaza Hifadhi ya Taifa ya Kitulo.

Amefafanua kuwa hifadhi hiyo imekuwa ikitangazwa katika matamasha mbalimbali ya Karibu Kusini, Kilifair na Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba na Nanenane na kwa njia ya kidigitali, mitandao ya kijamii, majarida na Safari Channel.

Kufuatia hatua hiyo Serikali imeanza kuboresha miundombinu ndani ya hifadhi hiyo ikiwemo kufanya ujenzi wa nyumba tatu za malazi ya watalii na pia inatarajia na kujenga nyumba mbili na kambi moja ya kuweka hema katika mwaka huu wa fedha 2023/2024, pamoja na kukarabati miundombinu ya barabara.

Kuhusu utatuzi wa migogoro ya mipaka kati ya hifadhi hiyo na wananchi, Mhe. Masanja amesema tathmini ilishafanyika na kulielekeza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuweka vigingi katika maeneo ambayo yameshaainishwa.