January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakazi wa Rufiji wapigwa msasa

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Wakazi wa Halmashauri ya Rufiji Mkoani Pwani wameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kutoa mafunzo ya mazao ya misitu huku wakiahidi kuwa elimu waliyoipata itatumika kuwanufaisha Wananchi wote wa Mkoa wa Pwani katika kulinda Maliasili za nchi pamoja na kufuga nyuki kibiashara

Akizungumza leo wilayani Rufiji kiongozi wa ziara ya Mafunzo ya Utekelezaji wa Sera ya Misitu na Sera ya Ufugaji Nyuki kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Emmanuel Msoffe amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa wakazi wa Rufiji ambapo yatakwenda kuwasaidia kujua namna bora ya kuhifadhi na kutunza misitu kwa faida ya kizazi cha sasa na cha baadae.

Amesema Wizara ya Maliasili na Utalii imeamua kutoa mafunzo hayo kwa Wana Rufiji ili kuwapa uelewa mkubwa ambao utawasaidia wakazi hao juu ya namna bora ya kuifanya misitu kuwa endelevu

Msoffe amesema mara baada ya mafunzo hayo Wadau wamewaelezea changamoto na mafanikio mbalimbali wanayoyapata katika shughuli za uhifadhi lakini hata hivyo Wadau hao wamekiri kuwa wamépata uelewa mkubwa kupitia mafunzo hao ambayo yatawasaidia kubadilishana mawazo na uzoefu ambao watautumia katika kutekeleza shughuli za Misitu na Nyuki

Aidha, amesema mbali na kuelezwa changamoto zinazowakabili wakazi wa eneo hilo ikiwemo ya wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba yao pamoja na uvunaji haramu wa mazao ya misitu, ziara imekuwa na mafanikio makubwa .

Kwa upande wake Mdau wa Misitu kutoka wilaya ya Rufiji, Mohammed Salum ameipongeza Wizara kwa kufanya kazi kubwa ya kutoa elimu ya mazao ya misitu kwani itawasaidia kupata kipato cha mtu mmoja mmoja na kuleta maendeleo kwa taifa kwa ujumla

“” Faida tunaijua na tumeiona, elimu mnayotupa mara kwa mara kuhusiana na uhifadhi wa misitu na ufugaji nyuki inatusaidia sana kuwa mabalozi wazuri wa uhifadhi hapa nchini ” amesema Mohammed.

Ameongeza kuwa elimu ya kulinda misitu na kufuga nyuki ambayo wamekuwa wakipewa mara kwa mara imekuwa msaada mkubwa kwani kwa sasa mazao ya misitu yamekuwa yakiwaingizia kipato kilichowawezesha kujenga ofisi ya kijiji, shule, wodi ya kina mama pamoja na maabara.