May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Mwinyi kukijenga Chama kiunchumi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameahidi kukijenga chama kiuchumi kwa kuimarisha miundombinu wezeshi ya utendaji kwa watendaji wake ili kuboresha ufanisi ndani ya chama hicho.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo alipozungumza kwa mara ya kwanza na viongozi wa chama cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya mashina, majimbo, wilaya, hadi Mkoa, kwenye ukumbi wa Piccadilly, uliopo Kombeni, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Makamu Mwenyekiti huyo alieleza ili chama kifanye kazi zake kwa ufanisi ni lazima kiwe na vifaa vya kutendendea kazi vikiwemo vyombo vya usafiri na vifaa vya kisasa vya ofisini vyenye hadhi na umri wa chama hicho.

“Tutafanya kila linalowezekana kukijenga chama kiuchumi” alieleza Mamamu mwenye kiti huyo.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alikiahidi chama kukitendea makubwa zaidi wakati huu wa uongozi wake ikiwemo kujenga ukumbi mkubwa wa mikutano ambao chama utajivunia nchi nzima na kueleza maendeleo makubwa yaliyofikiwa Zanzibar ni utekelezaji wa Ilani ya chama ambayo kwasasa imefikia nusu ya utekelezaji wa ahadi zake na kwamba sehemu ndogo iliyobaki itakamilishwa kwa wakati.

Alisema, CCM ina rasilimali nyingi nakueleza baadhi ya rasilimali hizo hata bado hazijatendewa haki.

Akizungumzia suala la umoja na mshikamo ndani ya Chama hicho, Makamu Mwenyekiti huyo, alionya mfarakano na mgawanyiko ndani ya Chama na kuwaasa wanachama wawe kitu kimoja ili kuongeza nguvu ya chama chao.

Alisema wakati wa chaguzi zote huibuka makundi mbalimbali yenye dhamira na maslahi tofauti hivyo, aliwaasa wana CCM kurejesha umoja na mshikamano mara baada ya uchaguzi kukamililka.

Aidha, alionya endapo ikitokea hali ya mgawanyiko wa makundi ndani ya chama hicho, ameziagiza kamati za maadili kuchukua hatua kali za nidhamu na kuhakikisha nidhamu na mshikamano ndani ya chama unarejea.

Akizungumzia suala la uhai wa chama, Makamu Mwenyeki CCM, Rais Dk. Mwinyi, aliwataka viongozi wenye dhamana kwa mujibu wa nafasi zao ndani ya chama hicho, kutekekeza jukumu na kuongeza wanachama wepya ili kuendelea kukipa uhai chama hicho kiendee kushika dola.

“Mtaji wa chama chetu ni kuongezeka wanachama wepya, kadi ziwepo za kutosha” alisisitiza Makamu Mwenyekiti huyo.

Vilevile, Rais Dk. Mwinyi aliwahimiza wana CCM kulipa michango kwa wakati badala ya kusubiri hadi vipindi vya uchaguzi vikaribie.

Katika hatua nyengine, Rais Dk. Mwinyi, aliagiza chama kuwapa mafunzo ya uongozi watendaji wa ngazi zote walioshinda kwenye uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana pamoja na kujipanga tena kwaajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Naibu Katibu mkuu CCM, Zanzibar Dk. Muhamed Said Muhamed Dimwa, akizungumza kwenye hafla hiyo, alieleza CCM haitajibu maneno wanayorushiwa na wapinzani badala yake wataendelea kuitekeleza Ilani ya chama chao kwa kuboresha maendeleo ya nchi na watu wake na kuahidi kutowafumbia macho wenye dhamira ya kukwamisha ilani ya chama hicho.

Nae, Mjumbe wa Kamati ya siasa ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa aliwaasa wanachama wa CCM kuwachagua viongozi wenye sifa na weledi wa kuwatumikia sio kuwanunua viongozi wakati wa chaguzi za chama hicho, pia alieleza kuna ushirikiano wa moja kwa moja baina ya chama na Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake, Tanzania Zainab Khamis Shomari, alieleza ahadi ya wanawake na kinamama Tanzania bado ipo palepale ya kurejesha ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi mkuu wa 2025.

Pia aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kuwajengea heshima wanawake kwa kuwapa fursa ya uongozi kwenye sekta mbalimbali.

Naye, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi Kichama, Muhamed Rajab Soud, alishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kuufungua kimaendeleo mkoa huo kwa kuwepo na wawekezaji mbalimbali jambo alilolisifu wamewajengea heshima kubwa kwenye Mkoa wao.

Huo, ulikua mkutano wa kwanza wa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. Mwinyi na viongozi wa chama hicho kwa ngazi za mashina, majimbo, wilaya, hadi Mkoa, tokea kumalizika wa chaguzi za chama hicho, mwishoni mwa mwaka jana.