May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakandarasi Zanzibar watakiwa kusimamia mikataba

Na Haji Mtumwa, TimesMajira Online Zanzibar

WAKANDARASI wa Miradi ya Maendeleo visiwani Zanzibar wametakiwa kusimamia Mikataba waliofunga na Wizara husika ili kukamilisha kwa wakati uliopangwa Miradi hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla jana wakati wa muendelezo wa ziara ya kukagua Miradi inayojengwa kwa fedha za Mkopo wa ahueni ya uviko 19 katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema, sijaridhishwa na baadhi ya Wakandarasi walio nje ya muda ambao wanasababisha kuchelewa kwa kukamilika Miradi hiyo ambayo inaendelea na ujenzi katika maeneo mbalimbali visiwani hapa.

“Kwa kweli sikuridhishwa na uendeshaji wa Miradi hii ambayo kasi yakeinaonekana ni ndogo, niwaombe sana Wakandarasi kuhakikisha kufuata mikataba yenu Ili mmalize ujenzi kwa wakati.

“Hata hivyo nimesikitishwa na baadhi ya watendaji wa Wilaya na Halmashauri kutokushirikiana kwa pamoja katika kusimamia na kufuatilia miradi hiyo jambo ambalo serikali imekwisha elekeza viongozi hao kuwa karibu na wakandarasi waliokabidhiwa miradi hiyo,” alisema Abdullah.

Sambamba na hayo Abdulla ameuagiza uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya Amali Zanzibar, kuajiri Mshauri elekezi ili kusimamia ubora wa majengo ya shule yanayoendelea kujengwa.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Muhamed Mahmoud ameahidi
kusimamia miradi yote iliyomo katika Mkoa huo kumalizika kwa wakati na kwa kiwango kilichokusudiwa.

“Serikali ya Mkoa itasimamia Maagizo yote yaliyotolewa na serikali kuu, katika kuona kila mmoja anatekeleza vyema majukumu ake katika kufanikisha na majengo yanayojegwa,” alisema

Kwa upande wake Kamishna wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar Khamis Bakar Khamis, amemuhakikishia Abdulla Kuwa ujenzi unaendelea vyema chini ya ukandarasi wa Chuo hicho na kuahidi majengo ya shule ya Mkwajuni na mejengo mengine kukamilika kwa wakati na kwa kiwango kilichokusudiwa.