May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakandarasi wataja kero ujenzi miradi ya maendeleo

Na Cresensia Kapinga, Songea.

BAADHI ya wakandarasi wa barabara wilayani Mbinga mkoani Ruvuma wameiomba Serikali kufuta baadhi ya tozo ambazo inadaiwa kuwa ni kero kwenye kazi zao za ujenzi wa miradi ya maendeleo ya barabara.

Wamesema hawaoni sababu ya tozo aina moja kulipwa maeneo matatu wakitolea mfano kama tozo ya kuchimba kifusi au kokoto kulipwa ofisi ya madini, kisha kwenda kulipia halmashauri badala yake wameshauri Serikali ibakishe eneo moja la kulipia tozo hiyo kama ni halmashauri au ofisi za madini.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Ovans Construction ya wilayani humo, Valens Urio amesema ni vyema serikali ikaondoa utitiri wa tozo kwenye miradi ya maendeleo ili wakandarasi waweze kuomba kazi kwa wingi na itasaidia miradi mingi kumalizika kwa wakati.

“Niombe Serikali yangu tukufu chini ya uongozi wa Rais wetu Samia Suluu Hassan kuona umuhimu wa tozo zilizopo tulipie eneo moja kama ni ofisi za madini au halmashauri na si vinginevyo.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Ovans Construction ya Wilayani Mbinga, Valens Urio akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki ofisini kwake juu ya changamoto wanazokutana nazo kwenye kazi zao ikiwemo utitiri wa tozo. Cresensia Kapinga.

Hii itatusaidia sana wakandarasi kuondoa sintofahamu iliyopo na wakandarasi wengine kukatishwa tamaa kutokana na uwingi wa tozo na fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi hiyo ni ndogo na haukidhi mahitaji ya mradi,”amesema Urio.

Urio amesema kutokana na jigrafia ya Wilaya ya Mbinga na Nyasa ilivyo inakuwa ngumu sana kupata vibarua wa kufanya kazi unapowatoa maeneo mengine inasababisha kutoelewana na wakazi wa maeneo yale, jambo ambalo linasababisha kupandishiwa kwa gaharama za maeneo ya uchimbaji wa vifusi ama kokoto kuwa kubwa.

Baadhi ya wananchi wamepongeza kazi zinazofanywa na wakandarasi wilayani humo ila wameomba TARURA kuwawekea mifereji kwani barabara nyingi zinaharibika kipindi cha masika kutokana na kukosekana kwa mitaro.

Moja ya barabara ya kiwango cha rami iliyojengwa na mkandarasi, Ovans Construction kutoka wilayani Mbinga.

Naye kaimu meneja wa TATURA Wilaya ya Mbinga Mhandisi Amos Agastin amesema kazi walizozifanya kwa sasa ni kutengeneza barabara kuweka karavatai, kujenga madaraja na bajeti ijayo wataendelea na kazi ya uchimbaji na ujengaji wa mitaro na watahakikisha barabara zote zinapitika kipindi chote.