November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakala vipimo Kinondoni ataka kanuni za vipimo kuzingatiwa

Na Bakari Lulela

WITO umetolewa na Wakala wa Vipimo Mkoa wa Kinondoni (WMA) Dar es Salaam wananchi kuendelea kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo ili kumfanya mlaji Kupata matokeo chanya pindi katika maeneo ya biashara.

Akizungumza Mkoani humo, Meneja wa Wakala wa vipimo Mkoa wa Kinondoni Charles Mavunde amesema kumekuwa changamoto kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kupunja kupitia matumizi yasiyo sahihi ya vipimo.

“Wakala wa Vipimo tuna majukumu makuu manne ya kisheria ambayo ni pamoja na kuhakiki vipimo vyote vinavyotumika katika masuala ya biashara, mazingira, usalama na afya,” amesema Mavunde

Aidha Mavunde amesema kwamba Wakala hao kwa mujibu Sheria ya Vipimo Sura 340 wataendelea kusimamia majukumu mengine ikiwemo kufanya ukaguzi wa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa katika viwanda vya ndani, kutoa elimu ya matumizi sahihi ya vipimo sambamba na kufanya kaguzi mbalimbali kwa wateja watumiao vipimo walio masokoni, madukani mabuchani, viwandani na maeneo mbalimbali ambapo kuna matumizi ya Vipimo.

Hata hivyo Meneja wa Wakala hao amesema kuna bidhaa zitokanazo na nishati ya mafuta na gesi ambazo zinahitaji uwiano sahihi katika upatikanaji wake na umuhimu wa vipimo hivyo ni mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi yetu. Matumizi sahihi ya Vipimo inatusaidia katika upatikanaji wa takwimu sahihi katika viwanda, kilimo na ufugaji, madini. Pia husaidia upangaji bei katika nishati ya gesi na mafuta na katika matumizi ya maji na umeme, uzalishaji sahihi viwandani.

Wakala wa Vipimo Mkoa wa Kinondoni wanasisitiza kwamba watu wote wanaofanya biashara kwa kutumia vipimo kwa wananchi kuendelea kuhakiki vipimo vyao kila mwaka hatua ambayo wao kama Wakala hufanya kaguzi mbalimbali kuhakikisha kila mfanyabiashara anazingatua matumizi sahihi ya vipimo ili kuleta tija na manufaa kwa mlaji.

Kutokana janga la UVIKO 19 lililoikumba dunia, Wakala wa Vipimo Mkoa wa Kinondoni tunachukua tahadhari kwa kuwaambia wateja wetu kuwa tunaendelea kupokea na kuzingatia maelekezo kutoka kwa wataalamu wetu wa afya kujilinda na Uviko 19 kwa kutekeleza matumizi sahihi ya vitakasa mikono, kuna wa kwa maji tiririka, kuvaa barakoa na kupata chanjo dhidi ya UVIKO 19.

Alihitimisha kwa kauli mbiu “miaka 60 ya uhuru tuzingatie matumizi sahihi ya vipimo kukuza uchumi wa viwanda”.