May 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wabunge na Wajumbe wa Baraza Kuu la Chama Cha Wananchi CUF Taifa wakiwa katika gari la polisi baada ya kukamatwa wakiwa wanaendesha vikao vya ndani  wilayani Pangani. Picha na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

Wajumbe wa Baraza Kuu Cuf wakamatwa na Polisi Pangani.

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga,

WABUNGE watatu na wajumbe wanne wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama cha Wananchi (CUF) wamekamatwa Jeshi la Polisi Wilaya Pangani wakiwa kwenye vikao vya ndani vya uhamasishaji wa wanachama kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Wajumbe hao wamekamatwa na kushikiliwa kwa takribani saa nne na kuachiliwa kwa dhamana baada ya kufanya vikao vinne katika kata tofauti za Wilaya Pangani.

Waliokamatwa na polisi ni pamoja na Wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi CUF Taifa Kapasha wa Kapasha, Thomas Malima kutoka Musoma, Abdul Kambaya kutoka Dar es Salaam.

Wengine ni Yassin Mrotwa kutoka Mbeya pamoja na Mkurugenzi wa Habari wa Jumuiya ya Wanawake CUF Taifa Sonia Magogo ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu Handeni pamoja na Katibu wake Irene Magoa.

Wajumbe wengine waliokuwepo eneo hilo la tukio ni pamoja na Mbunge wa Tanga, Mussa Mbaruk, na Rukia Kassim kutoka Visiwani Pemba.

Mbunge Mbaruk amekiri kukamatwa na Jeshi la Polisi lakini baada ya kuwaelewesha polisi walikiri kuchelewa kupata taarifa za wao kufanya mikutano yao ya ndani. Amesema baada ya kuelewana waliruhusiwa kuendelea na mikutano yao ya ndani wilayani humo kwa muda wa siku mbili.

Naye Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga, Blasius Chatanda amesema hakuna aliyekamatwa wajumbe hao walitaka kufanya mikutano bila kufuata taratibu. Amesema ili kuimarisha usalama walilazimika kuwaita na kuwaeleza wapi wamekosea na nini walipaswa kufanya na kueleza kuwa hakuna aliyekamatwa wala kufanyiwa mahojiano.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Itifaki na Udhibiti wa Mafunzo CUF Taifa, Masoud Omary Mhina ameliasa Jeshi la Polisi kuacha kutumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuwanyima kufanya siasa za kweli.

Mkurugenzi Masoud amdesema hiki ni kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa kuwapata Madiwani, Wabunge na Rais hivyo hawawezi kupata watu hao bila ya kukutana na wanachama.