November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wajasiriamali milioni 1.7 wanufaika na mikopo inayodhaminiwa na PASS TRUST

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Jumla ya wajasiriamali milioni 1.7,wamefaidika na mikopo yenye thamani ya trilioni 1.219 kutoka kwa taasisi mbalimbali za fedha iliyodhaminiwa na Taasisi ya kuwezesha sekta binafsi ya kilimo(PASS TRUST).

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa PASS TRUST Adam Kamanda kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo Yohane Kaduma,katika mkutano wa PASS TRUST na wadau wa kilimo uliofanyika mkoani Mwanza wenye lengo la kuongeza uelewa kwa wadau.

Kamanda amesema, taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 2000 nchini hapa kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa huduma za kifedha na kibiashara kwa wajasiriamali wa bidhaa na huduma katika sekta ya kilimo,Mifugo na uvuvi ambapo tangu kuanzisha kwake jumla ya wajasiriamali milioni 1.7 wamenufaika.

Amesema,kwa kutambua unyeti wa sekta ya kilimo nchini mpaka kufikia mwaka jana jumla ya biashara zipatazon532,798 zinazojihusisha na mazao na huduma kwenye kilimo zimenufaika kupitia dhamana zetu na huduma za maendeleo ya biashara katika mikoa yote nchini ambazo zimeweza kuboresha na kupanua wigo wa biashara za mazao ya kilimo,mifugo na Uvuvi nchini na kuzalisha ajira takribani milioni 2.6.

“Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa takribani asilimia 31 ya mikopo yote ya kilimo nchini imewezeshwa na udahamini wa PASS ambapo Kanda ya Ziwa ni moja ya Kanda muhimu katika sekta ya kilimo nchini kutokana na takwimu za mwaka 2021 pekee jumla ya wakulima na wajasiriamali 37,717 ambao kati yao 12,277 ni wanawake na wanaume 25,440 walinufaika na huduma zetu hii ni sawa na asilimia 25 ya mikopo tuliodhamini kwa mwaka 2021,” amesema Kamanda.

Pia amesema,kutokana na maboresho yanayoendelea kufanywa na wadau mbalimbali zikiwemo benki,juhudi za serikali pamoja na huduma yao ya kidijitali wanatarajia kuwafikia na kuwahudumia wakulima,wafugaji,wavuvi na wajasiriamali wengi zaidi katika mnyororo wa thamani.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel,akizungumza wakati akifungua mkutano huo amesema,mkutano huo ni nafasi kubwa ya kujadiliana na kupanga mipango na mikakati ya kutatua changamoto zinazowakabili wakulima,wafugaji, wavuvi na wasindikaji hivyo amewahimiza wananchi kuchukuliwa taasisi ya PASS kuwa ni fursa mojawapo itakayowezesha kurahisisha maendeleo.

Mhandisi Gabriel,amesema Kwa kutambua wakulima wengi ni wadogo na bado wanatumia teknolojia duni,kupitia hali hiyo wataweza kuweka mazingira rafiki zaidi ya kuwafikia wadau wengi wa sekta ya kilimo kundi ambalo kwa muda mrefu limekuwa haliwezi kuzifikia taasisi za kifedha kwa ufanisi

“Serikali ya Mkoa itawapa PASS ushirikiano wa kutosha ili wananchi wapate huduma hizi muhimu,nataka taasisi hii kupanua wigo wa kujenga uelewa kwa kufanya mikutano kama hii katika ngazi mbalimbali ili kuwafikia wakulima wengi zaidi,hii itasaidia kuharakisha upatikanaji wa huduma bora kwa kutumia za uwepo wenu na benki mbalimbali kwa ufanisi,” amesema Mhandisi Gabriel.

Mmoja wa wanufaika wa PASS TRUST,ambaye anajishughilisha na ufugaji wa nguruwe na kilimo Venance Barandaje,amesema awali changamoto ilikuwa ni upatikanaji wa mbegu bora lakini pia na elimu kuhusu chakula bora kwa ajili ya malisho ya nguruwe ni gharama sana na inahitaji mtaji mkubwa na kipato cha mara kwa mara.

“Wakati naanza ufugaji sehemu kubwa niliyokuwa natumia mshahara,mwaka 2018 niliota mbegu za kisasa na katika kutaka kukuza mradi nikaunganishwa na PASS TRUST ambayo umenisaidia kukua na kupanua mradi wangu baada ya kufahamu mahitaji ya chakula na kuzalisha wanyama kiasi gani,,kweli inawezesha watu wote ambao wapo katika mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo,mifugo na Uvuvi cha msingi ni kujua tathimini ya mradi wako” amesema Barandaje.

Naye Happiness Kishoa, amesema baada ya kuwezesha kupata mkopo amefanikiwa kuongeza mifugo pamoja na kuanza kifuga ng’ombe huku akisema ili kufanikiwa ni kufanya uthubutu,kujiamini na kufanya kitu ukiwa unakipenda pamoja na kuacha na dhana kuwa mtu aliyeshindwa ndio anapaswa kulima.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel, akizungumza wakati akifungua mkutano wa PASS TRUST na wadau wa kilimo wenye lengo la kutoa uelewa kwa wadau, uliofanyika mkoani Mwanza.picha na Judith Ferdinand
Baadhi ya wadau waliohudhuria mkutano wa PASS TRUST na wadau wa kilimo wenye lengo la kutoa uelewa kwa wadau, uliofanyika mkoani Mwanza.picha na Judith Ferdinand
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa PASS TRUST Adam Kamanda akizungumza katika mkutano wa PASS TRUST na wadau wa kilimo uliofanyika mkoani Mwanza wenye lengo la kutoa uelewa kwa wadau.picha na Judith Ferdinand